RC WILBERT IBUGE: MASHUJAA WA VITA VYA MAJIMAJI WATUHAMASISHE KUFANYA KAZI | Tarimo Blog

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Wibert Ibuge akizungumza na wakazi wa Songea kwenye Tamasha la kumbukizi ya Miaka 115 ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni linalofanyika Mjini Songea Mkoa wa Ruvuma.



Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Wibert Ibugea akipata maelezo kwenye moja ya banda la washiriki kwenye Tamasha la kumbukizi ya Miaka 115 ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni linalofanyika Mjini Songea Mkoa wa Ruvuma.



Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Wibert Ibuge akisalimiana na Chifu wa Wangoni Emanuel kwenye Tamasha la kumbukizi ya Miaka 115 ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni linalofanyika Mjini Songea Mkoa wa Ruvuma .

……………………..

Na Sixmund Begashe

Watanzania wametakiwa kuwaenzi mashujaa wa Vita vya Majimaji kwa kukuza uchumi waTaifa na kutekeleza kwa vitendo maagizo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu sera ya “Tanzania ya Viwanda” na kukuza utalii Ukanda wa Kusini.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi Wibert Ibuge kwenye ufunguzi rasmi wa Tamasha la kumbukizi ya Miaka 115 ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni linalofanyika Mjini Songea Mkoa wa Ruvuma.

Balozi Ibuge amesema kuwa maadhimisho hayo ni chachu ya kuhamasisha wadau na jamii kushiriki katika maendeleo ya nchi hasa Mkoa wa Ruvuma kama hatua muhimu ya kuwaenzi Mashujaa waliopigania utu wa wananchi kwa vitendo.

Mkuu wa Mkoa huyo aliongeza kuwa sehemu ya Maadhimisho hayo itakuwa ni kutembelea eneo la kijiji cha Maposeni kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijijini, mahali ambapo maji ya Vita vya MajiMaji yalianza kutolewa na Nduna Mkomanile na kuanza kutumiwa na Mashujaa wa Vita vya Maji Maji.

“Kijiji cha Maposeni ni makazi ya Chifu Emmanuel Zulu ambaye ni Chifu wa 5 wa kabila la Wangoni. Chifu, amewaalika Machifu wengine kutoka Mikoa mingine nje ya Ruvuma kama vile Njombe, Iringa, Mbeya, Tabora, Mwanza, Lindi na Mtwara. Huko kutakuwa na sherehe za Ngoni Day” Balozi Ibuge

Katibu Mkuu wa Baraza la Makumbusho Mila na Desturi Mkoa wa Ruvuma Mzee Abasi Chitete amesema wao kama wazee wa Mila wa Mkoa huo wameona ni vyema kuhakikisha watoto na wajukuu zao wanarithi urithi adhimu wa Mashujaa wa Vita vya Majimaji na Utamaduni wao.

“Sisi ni wazee, ndio tunaishia ishia sasa, tutakao waacha ni hawa watoto, sasa tumeamua kuhakikisha watoto hawa wanaielewa vyema historia ya mashujaa wetu waliolala hapa na wote waliopgania utu wetu, lazima wawe wazalendo ili taifa hili liendelee kusonga mbele” Mzee Chitete

Akizungumzia maandalizi na matarajio ya maadhimisho hayo, Mhifadhi Makumbusho ya Majimaji Bw. Balthazar Nyamusya amesema yamenda vizuri na taasisi nyingi za serikali na binafsi zimejitokeza kushiriki pamoja na wananchi wajitokeze kwa wingi kushuhudia maadhimisho hayo.

“Nimatarajio yetu kuwa siku za mbeleni Tamasha hili litakuwa kubwa kama matamasha mengine makubwa nchini, yaani kipindi hiki cha maadhimisho hapa Songea kufurike wageni wengi wa ndani na nje ya nchi hasa wanaruvuma wenyewe waliopo mikoa mingine waje na watoto wao kuburudika na kujifunza utamaduni wao” Bw. Nyamusya

Maadhimisho hayo ya Mashujaa wa Vita vya Majimaji na Utalii wa Utamaduni hufanyika kila mwaka Mjini Songea kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi za Serikali na binafsi, wazee wa Mila na Desturi Mkoa wa Ruvuma, Machifu wa Makabila mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2