AG FELESHI ASHIRIKI MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO VIONGOZI WA BUNGE | Tarimo Blog


Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeanda mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati ya Uongozi, Makamu Wenyeviti wa Kamati, na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge.

Mafunzo hayo ya siku tano yameanza leo Jumatatu na yanafanyika katika Ofisi Ndogo ya Bunge Visiwani Zanzibari. Mgeni rasmi alikuwa ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Aksoni .

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi ( Mb) ni miongoni mwa viongozi wanaoshiriki mafunzo hayo akiwa ni Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge.

Katika siku ya kwanza ya mafunzo hayo, mada iliyowasilishwa kwa washiriki ilihusu madaraka, majukumu, mipaka ya utendaji kazi, uzoefu na changamoto na uendeshaji wa Tume ya Utumishi wa Bunge na Kamati ya Uongozi.

Mada hii iliwasilishwa na Mhe. Anne Makinda Spika Mstaafu wa Bunge la Jamburi ya Muungano wa Tanzania huku wadadisi wa mada wakiwa ni Mhe. Pandu A Kificho, Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi na Mhe. Pius Msekwa Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania..

Aidha mada nyingine iliyowasilishwa katika siku ya kwanza ni pamoja na Bima ya Maisha iliyowasilishwa na Shirika la Bima la Taifa ( NIC).

Kwa mujibu wa ratiba ya mafunzo hayo, kesho ( jumanne) Washiriki hao wataelimishwa na kujengewa uwezo kuhusu; uzoefu, changaoto na mbinu za uendeshaji bora wa vikao vya Bunge la Vyama Vingi vya Siasa.

Mada hii itawasilishwa na Mhe. Pius Msekwa, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku wadadisi wa mada hiyo wakiwa ni Mhe. Anne Makinda, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe Pandu Kificho Spika Mstaafu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar .

Aidha mada nyingine itakayowasilishwa na kujadiliwa wakati Mafunzo hayo ni juu ya Uratibu wa shughuli za Bunge na Serikali; uzoefu na changamoto.

Mada hii itawasilishwa na Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais ( Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora).

Washiriki wa Mafunzo hayo pia watajengewa uwezo kuhusu misingi ya uongozi na utawala bora, mada itakayotolewa na Mtaalamu kutoka Uongozi Institute.

Viongozi hao wa Bunge pia watajengewa uwezo kuhusu masuala ya Diplomasia, Itifaki, Miiko na masuala muhimu yanayojenga Haiba ya Viongozi. Mada hii itawasilishwa na Mtaalamu kutoka Chuo cha Diplomasia. Vilevile Viongozi hao wataelimishwa kuhusu huduma za Bima ya Afya kwa wabunge, uzoefu, mafanikio na changamoto.

 


Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi ( Mb) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wanaoshiriki mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo Kamati ya Uongozi wa Bunge ambayo Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni Mjumbe, Makamu wenyeviti wa Kamati na Tume ya Utumishi wa Bunge. Mafunzo hayo ya siku tano yanafanyika katika Ofisi Ndogo ya Bunge Zanzibar

 


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2