Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Abdullah bin Zayed tarehe 13 februari 2022 ametembelea Banda la Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Mohamed Abdullah Mtonga ambaye pia ni Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania kwenye Maonesho ya Expo 2020 Dubai.
Baada ya kuwasili kwenye banda hilo na kutembezwa, Mhe. Zayed aliipongeza Tanzania kwa kuandaa Banda lenye mvuto na linaloonyesha vivutio vya utalii pamoja na fursa zilizopo katika sekta mbalimbali kama za utalii, nishati, uchukuzi na madini.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi alimshukuru Mgeni wake kwa kuchagua kutembelea banda la Tanzania ikiwa ni moja ya nchi 192 zinazoshiriki maonesho hayo. Aidha, aliishukuru Serikali ya UAE kwa kuandaa vizuri Maonesho makubwa ya Expo 2020 Dubai, licha ya uwepo wa changamoto ya kuenea kwa ugonjwa wa COVID -19.
Ushiriki wa Tanzania unatarajiwa kuwa na matokeo chanya na kuongeza idadi ya Watalii watakaoitembelea Tanzania, wawekezaji, mitaji pamoja na masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini. Katika Maonesho haya, Tanzania ni miongoni mwa nchi 50 ambapo kwa mara ya kwanza zinashiriki kwenye mabanda pekee yaliyojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya UAE.
Katika hatua nyingine, Ubalozi wa Tanzania, UAE utasherehekea Siku ya Kitaifa (National Day) tarehe 27 Februari 2022. Sherehe hizo zitapambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo Kongamano kubwa la Biashara na Uwekezaji litakalofanyika kwenye Ukumbi wa Ballon, Hoteli ya Jumeirah Beach tarehe 27 Februari 2022.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Abdullah bin Zayed alipowasili kwenye Banda la Tanzania katika Maonesho ya Expo 2020 Dubai na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Mohamed Abdullah Mtonga
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Abdullah bin Zayed akiangalia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa nchini inayooneshwa kwenye Banda la Tanzania katika Maonesho ya Expo 2020 Dubai.
Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Mhe. Mohamed Abdullah Mtonga akibadilishana mawazo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Sheikh Abdullah bin Zayed alipowasili kwenye Banda la Tanzania katika Maonesho ya Expo 2020 Dubai.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment