NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete wamewataka wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Mwaka huu kuripoti kwenye shule walizopangiwa Ili waweze kuendelea na masomo yao.
Kikwete alisema hayo kwenye ziara ya kukagua Maendeleo ya Jimbo la Chalinze lililopo Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani, ambapo alisema kuwa, kati ya wanafunzi 5300 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Mwaka huu, wanafunzi 1000 hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa.
Alisema zoezi la kuhakiki wanafunzi hao linaendelea ili msako wa kuwatafuta na kuwarudisha shuleni Kwa ajili ya kuendelea na masomo.
Alisema kuwa, Serikali imetoa Utaratibu wa elimu bure kwa kila mwanafunzi Ili kuhakikisha wanafunzi wote wanapata fursa ya kuendelea na masomo, jambo ambalo litasaidoa kuinua uchumi wa taifa Kwa kuwa na wasomi wengi.
" Kila mtoto ana haki ya kupata elimu bure, hivyo basi wazazi na walezi mnapaswa kuwapeleka Watoto kusoma, ni lazima na sio hiyari, kila mmoja anapaswa kuwajibika," alisema Ridhiwani.
Aliongeza kuwa, Maendeleo ya nchi yanaletwa kwa wanafunzi kupata elimu, hivyo basi wazazi na walezi wanapaswa kuwa na mwamko wa kuhakikisha watoto wao wanasoma na walioacha wanarudi shule.
" Ninaomba watendaji wa kata na Mitaa kushirikiana na Maofisa elimu wa Halmashauri ili kufanya msako kwa wanafunzi walioshindwa kuripoti na kuwarudisha shuleni Ili waweze kuendelea na masomo yao," alisema Kikwete.
Alisema kuwa, wazazi na walezi wanatakiwa kutoa ushirikiano wakati wa zoezi la kuwasakata wanafunzi hao ili waweze kurudishwa shuleni.
Alisema kuwa, ikiwa wanafunzi watapata elimu, suala la Maendeleo litakua rahisi Kwa sababu watakua na uelewa.
" Kila mzazi na mlezi ana wajibu wa kuwaelimisha watoto ili waweze kupata elimu,kwa sababu ni haki yao ya msingi na kwamba elimu ni bure,jambo ambalo litachangia kupata Maendeleo," alisema.
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano wa kuwapata wanafunzi hao Ili waweze kurudi shule.
Hata hivyo, Diwani wa Kata ya Miono,Juma Mpwimbwi alisema kuwa, jando, unyago,kuolewa na utoro ni miongoni mwa sababu zinzochangia kuongezeka kwa Watoto walioshindwa kuripoti shule hasa katika msimu wa Mwaka huu.
Alisema kuwa, baadhi ya wazazi na walezi wanashiriki Kwa namna Moja au nyingine ya kuwaachisha watoto wao ili waende kuolewa Kwa wale wa kike huku wakiume kujishughulisha na shughuli mbadala kinyume na Utaratibu, hali ambayo imechangia watoto kutoripoti.
Hata hivyo,Kaimu Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Chalinze,Irene Joseph alisema kuwa,idadi kubwa ya wanafunzi hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo utoro, kuolewa na Unyago, hali ambayo inarudisha nyuma Maendeleo ya wananchi katika sekta ya elimu.
" Tumeanza zoezi la kuwafuatilia wanafunzi wote wasioripoti kwenye shule,zoezi hilo litaendelea na wale wazazi au walezi ambao watabainika kuwazuia kurudi shule watachukuliwa hatua," alisema.
Alisema kuwa, licha ya Serikali kutoa elimu kwa wananchi ya kuwataka wanafunzi hao kurudi shule,Lakini bado mwamko ni mdogo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment