Saudia Yaonesha nia kuwekeza kwenye Mwendokasi | Tarimo Blog



Na.Mwandishi Wetu.

Nchi ya Saudiarabia imeonyesha nia ya kufanya uwekezaji mkubwa katika mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) katika uendeshaji wa Mabasi, Teknolojia pamoja na mifumo ya uendeshaji kutokana na uzoefu wa miaka mingi walio nao katika sekta hiyo, lakini pia kutokana na Tanzania kuwa na mazingira mazuri na tulivu kwaajili ya uwekezaji.

Akizungumza na Menejimenti ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka pamoja na wawakilishi wa makampuni ya uwekezaji kutoka Saudiarabia, Balozi wa Tanzania nchini Saudiarabia Mh. Ally Mwadini amesema ujumbe huo umeonyesha nia ya kuja kuwekeza katika sekta ya usafirishaji hasa katika mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka kutokana na mazingira wezeshi yaliyopo Tanzania ambayo yanawahakikishia wawekezaji uhuru wa kuwekeza.

“Leo tumekuja kwa ajili ya kuona ni namna gani Saudiarabia inaweza kushiriki katika mradi huu wa Mabasi Yaendayo Haraka maarufu kama mwendokasi, hii inatokana nan chi ya Saudiarabia kuwa na uzoefu katika uendeshaji wa Miradi kama hii, lakini pia kwakua Tanzania ni nchi ya Amani na utulivu na yenye watu wakarimu pamoja na mazingiza wezeshi yaliyopo katika uwekezaji” Alisema Balozi Mwadini.

Amesema Tanzania ina umuhimu mkubwa sana kibiashara na uwekezaji katika ukanda huu wa Afrika kwani imepakana na nchi nyingi ambazo hutegemea huduma na bidhaa zake kupitia hapa nchini suala ambalo linawafanya wawekezaji kuona fursa hiyo na kuvutiwa kuja kuwekeza.

“Nimeambatana na wawakilishi wa kampuni ya Saudiarabia Public Transport Company (SABTCO) pamoja na Taasisi ya Uwekezaji ambayo inahusika na kuwekeza nchini Saudiarabia pamoja na nje ya nchi lengo kubwa ni kuja kuona na kutathmini namna watakavyoweza kuja kujiunga na Tanzania katika kuendeleza sekta ya Usafirishaji pamoja na sekta nyingine ambazo watavutiwa nazo” Alisema Balozi Mwadini.

Balozi Mwadini alisema Saudiarabia ni nchi iliyoendelea na yenye mahusiano mazuri na Tanzania hivyo wameamua kuja kuunga mkono Juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mh.Samia Suluhu Hassan za kuwaletea Watanzania maendeleo.

Kwa upande wake mwakilishi wa Kampuni ya SABTCO Bw.Hassan Abduljawad alisema wameona mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ni eneo sahihi kwa wakati huu kutembelea na kuona namna wanavyoweza kuwekeza kwakua kuna awamu sita za mradi huo katika Jiji la Dar es Salaam jambo ambalo linahitaji uwekezaji wa watu wengi na wa fedha nyingi.

“Sisi tuna uzoefu wa kuendesha miradi kama hii kwa miaka mingi tumeona kwa awamu zote za mradi hapa Tanzania tunawez na sisi kuja kuwekeza katika moja ya awamu ili tuweze kutoa mchango wetu na uzoefu wetu kwa ajili ya watanzania” Alisema Bw. Abduljawad.

Ujio wa wawekezaji kutoka Saudiarabia ni moja ya Juhuzi zilizotokana na ziara ya Mh.Rais Samia Suluhu Hassan katika nchi za Ulaya na Falme za kiarabu za kutafuta wawekezaji kwaajili ya kuja kuwekeza katika sekta mbali mbali hapa nchini.

Aidha kituo cha uwekezaji Tanzania TIC kimekua mstari wa mbele katika kutafsiri maono ya Rais Samia ya kutaka kuona Tanzania inayokua kiuchumi kupitia uwekezaji wenye tija kwa kuendelea kuratibu na kuleta wawekezaji katika sekta mbalimbali ili kutumia fursa nyingi zinazopatikana nchini.




Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mh.Ally Mwadini akizungumza na wanahabari (Hawapo Pichani) Katika ukumbi wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Ubungo Maji Jijini Dar es Salaam baada ya kikao baina ya Wakala na wawekezaji kutoka Saudi Arabia, Machi 28, 2022.


Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia Mh.Ally Mwadini (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Katika ukumbi wa Wakala Ubungo Maji Jijini Dar es Salaam baada ya kikao baina ya Wakala na wawekezaji kutoka Saudi Arabia, Machi 28, 2022.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2