Na Eleuteri Mangi, WUSM- Dar es salaam
Serikali inaridhishwa na kuthamini hatua zinazochukuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) katika kujenga na kuboresha miundombinu rafiki ya michezo ili kuendelea kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana katika michezo mbalimbali nchini.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu ametembelea kujionea mradi wa ujenzi wa kituo cha michezo cha kisasa kinachojengwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa ufadhili wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu Yakubu ametembelea kituo hicho cha kitaifa cha mfano Februari 28, 2022 ili kujionea hatua zinazochukuliwa na TFF katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kujenga miundombimu ya mchezo nchini ikiwemo soka.
“Mradi huu ambao unatekelezwa na TFF kwa ufadhili wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ni mkubwa, una ghorofa tatu ambazo zinauwezo wa kuchukua vijana 72 kwa wakati moja na katika eneo hili yatakuwepo maghorofa ya namna hiyo saba, haya ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya TFF na FIFA” amesema Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu.
Katika kuhakikisha sekta ya michezo nchini inakua, Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema kuwa uendelezaji wa miundombinu ya michezo nchini ni kipaumbele cha Serikali ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imejipanga kujenga viwanja 56 katika shule mbalimbali nchi nzima ambavyo lengo lake ni kulea vipaji vya vijana katika michezo.
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha michezo nchini kwa kushirikiana na wandau mbalimbali ambapo imejipanga kuwa na kanda sita za vituo mahiri katika michezo nchini ambapo watashirikiana na wadau wa michezo ikiwemo TFF na wadau wengine ili kuhakikisha michezo yote inaendelezwa na kuibua vipaji vingi zaidi nchini.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema kuwa kituo hicho kitasaidia pia kutoa mafunzo kwa walimu na waamuzi wa soka watapata fursa ya kufundishwa ili kuondokana na malalamiko yanayotolewa na wadau wa michezo pamoja na mashabiki wa soka nchini.
Kwa pande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Bw. Wallesi Karia ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wanaopata ikiwemo kutembelea mradi huo kujione hatua waliyofikia ili kutimiza ndoto ya shirikisho hilo ya kuwa na vituo vya mfano ambavyo kwa sasa vinajengwa vituo viwili, kimoja kinajengwa Kigamboni jijini Dar es salaam na cha pili kinajengwa mkoani Tanga.
“Mradi wetu kwa eneo ya majengo tayari umekamilika kwa asilimia kubwa, kwa upande wa viwanja bado ujenzi unaendelea, kiwanja cha nyasi bandia kipo tayari bado kubandika nyasi ambazo nazo tayari zipo hapa, lakini kwa upande wa kiwanja cha nyasi za kawaida tunatarajia zitapandwa mwezi huu wa tatu ambazo zitatakaa kwa muda wa siku 40 na baadaye zitakatwa ili kusawazisha na kuanza kutumika” amesema Bw. Karia.
Rais huyo wa TFF amesema Shirikisho hilo linatarajia kukabidhiwa mradi huo wa awamu ya kwanza ifikapo mwezi Juni 2022 ili kuruhusu awamu ya pili ya ujenzi wa viwanja vingine hatua itakayoongeza wigo wa vijana wengi kupata mahali pa kufanyia mazoezi kwenye viwanja vyenye hadhi ya kimataifa.
Rais Karia ameseongeza kuwa kituo cha Kigamboni ni cha kitaifa ambacho kitakuwa kinatumiwa na timu za taifa kitakuwa na viwanja vinne, madarasa ya kufundishia na kujifunzia pamoja na hosteli za kulala wachezaji wakati lengo la ujenzi wa kituo cha Tanga ni kuwa cha mfano ambapo mikoa yote nchini inapaswa kuwa na vituo kama hicho.
Katika kuhakikisha maeneo yote nchini yanakuwa na miundombinu ya michezo, Rais Karia ametoa wito kwa mikoa na halmashauri zote nchini kushirikiana TFF na wadau wa michezo kujenga kituo kama kile cha Tanga mikoa na halmashauri zote nchini ili vijana wapate maeneo ya kufanya mazoezi na kuendeleza vipaji vyao katika soka.
. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu (wa kwanza kulia) akitembelea maeneo mbalimbali ya ujenzi wa mradi wa kituo cha michezo cha kisasa kinachojengwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa ufadhili wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) wakati wa ziara ya kutembelea kituo hicho Februari 28, 2022 Kigamboni jijini Dar es Salaam. Katikati ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Bw. Wallesi Karia.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu (wa tano kushoto) akioneshwa ramani ya eneo la ujenzi wa mradi wa kituo cha michezo cha kisasa kinachojengwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa ufadhili wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) wakati wa ziara ya kutembelea kituo hicho Februari 28, 2022 Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment