Na Fredy Mshiu
Hatimaye wananchi wa mtaa wa Kombo kata ya Vingunguti wameanza kupata huduma ya majisafi na salama baada ya Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA) kuanza zoezi la kuwaunganishia huduma ya maji wakazi wa maeneo hayo.
Hii imekuja mara baada ya mradi wa maji wa jamii uliokuwa unahudumia wananchi hao kukabidhiwa chini ya uendeshaji wa DAWASA na wananchi kuingiwa na hofu ya kutoendelea kupata huduma.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Vingunguti, ndugu William Kibeyo akizungumza katika mkutano wa wananchi aliwaondoa hofu wananchi juu ya huduma huku akiwaeleza kuwa mabadiliko hayo ya uendeshaji wa mradi yanatokana na takwa la kisheria na mabadiliko ya sheria namba 5 ya mwaka 2019 inayoitaka DAWASA kuhudumia maeneo yote ya kihuduma na shughuli za jumuiya na kamati kukabidhiwa kwenye Mamlaka.
"Nitake kuwatoa hofu, Serikali hii inayotuhudumia ndio ilileta mabadiliko ya uendeshaji wa kamati zetu za maji za mitaa na kata na sisi kama viongozi wa Wananchi hatuna budi kusimamia sheria hizi ili zitekelezwe. Tunawahakikishia huduma itaendelea kupatikana kwa ubora na viwango sahihi "ameeleza ndugu Kibeyo.
Ndugu Kibeyo ameongeza kuwa wananchi miundombinu ya maji ya kamati iliyojengwa na shirika la maendeleo la Plan International itaunganishwa katika mfumo wa maji wa DAWASA na wananchi wasioweza kumudu gharama za kuunganisha huduma ya maji majumbani basi wataendelea kuhudumiwa kupitia kizimba hicho kwa gharama iliyowekwa na EWURA.
"Gharama iliyowekwa na EWURA kwa ndoo ya maji ya Lita 20 ni Tsh 50. Hii itasaiida familia ambazo bado hazijajipanga vizuri kuomba huduma ya maji katika nyumba zao" alimalizia Ndugu Kibeyo
Kwa upande wake meneja wa mkoa wa kihuduma DAWASA Tabata, Mhandisi Boniface Ole amewaeleza wananchi kuwa zoezi la kufunga mita kwa wananchi waliositishiwa huduma kwa sababu ya kutojisajili DAWASA imeanza na leo jumla ya wananchi 29 wameomba kusajiliwa na wameshafungiwa huduma.
"Utaratibu wa Serikali ni lazima mtumiaji wa maji awe na dira inayoonyesha matumizi yake, hapa wengi walikua hawana dira na kupelekea kutumia huduma ya maji bila kulipia. Awali tulisitisha huduma na kuwasihi wananchi wajitokeze ili wajisajili DAWASA na kutambulika ili wafungiwe dira za Maji. Muitikio ni mzuri kwani kati ya wananchi 100 waliositishiwa huduma , tumeweza kuwarudishia wananchi 29 na zoezi linaendelea"ameeleza Mhandisi Ole.
Mhandisi Ole ametoa wito kwa wananchi ambao bado hawajajaza fomu wala kujisajili DAWASA wajitokeze Ili wafungiwe dira za maji na kuendelea kupata huduma kwa haraka.
Ndugu Aisha Ramadhan, Mkazi wa mtaa wa Kombo amesema hofu iliyokuwepo awali ni wasiwasi wa kutopata huduma baada ya mradi kukabidhiwa DAWASA. Ila baada ya elimu sasa wapo tayari kutumia maji ya DAWASA kama walivyoelekezwa.
"Sisi Maji ya DAWASA tunayahitaji sana, kwa maelezo tuliyopewa hapa leo ile hofu yetu imekwisha, tunawaomba DAWASA maji haya yaendelee kutoka na yasikatike mara kwa mara na tuwahakikishie kuwa kila mkazi wa kwa kombo hapa Vingungiti yupo tayari kutumia maji safi na salama DAWASA" ameeleza ndugu Aisha.
Mabadiliko ya uendeshaji wa kamati za maji zilizokuwa chini ya Halmsahauri zimefanyika kufuatia mabadiliko ya Sheria ya Maji namba 5 ya Mwaka 2019 ambapo miradi yote ya jamii itakabidhiwa katika Mamlaka za maji kwa usimamizi na uendeshaji wenye tija.
Mpaka sasa jumla ya miradi 295 iliyokuwa ya jamii/kamati za maji katika Jiji la Dar es salaam imekabidhiwa chini ya DAWASA kwa usimamizi na uendeshaji.
Meneja wa mkoa wa kihuduma DAWASA Tabata, Mhandisi Boniface Ole akizungumza na wananchi wakati wa zoezi la kuwaunganishia huduma ya maji mtaa wa Kombo kata ya Vingunguti
Meneja Mawasiliano DAWASA, Everlasting Lyaro akizungumza na wananchi wakati wa zoezi la kuwaunganishia huduma ya maji mtaa wa Kombo kata ya Vingunguti
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment