Afisa Elimu Mkoa wa Kagera, Bw. Khalifa Semaonge akikabidhi mpira kwa washiriki wa bonanza la michezo ngazi ya mkoa mjini Bukoba mwishoni mwa wiki. Anayeshuhudia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa muda wa Jambo for Development, Bw. Clemens Mulokozi.
Na Mwandishi wetu, Kagera
ZAIDI ya Shilingi Milioni 320 zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika shule saba katoka katika halmashauri za mkoa wa Kagera.
Miradi hii ni matokeo ya mashindano ya michezo yaliyoshirikisha shule mbalimbali katika wilaya hizo na kuhitimishwa katika bonanza kubwa la michezo kimkoa mwishoni mwa wiki mjini Bukoba. Shule zilizoshinda katika ngazi ya wilaya na zitakazofaidika na miradi hiyo ni kutoka katika halmashauri za wilaya za Karagwe, Kyerwa, Ngara, Misenyi, Bukoba, Bukoba Manispaa na Muleba.
Miradi hiyo itakayotekelezwa na shirika la Jambo for Development kwa ushirikiano na serikali na jamii inatarajia kufaidisha wanafunzi takribani 7,500 katika shule hizo. Shirika hilo litafadhili asilimia 60 ya miradi hiyo huku halmashauri za wilaya zitachangia asilimia 30 na jamii asilimia 10.
Akiongea wakati wa tamasha hilo la michezo mjini Bukoba, Afisa Elimu Mkoa wa kagera, Bw. Khalifa Semaonge aliyekuwa mgeni rasmi alipongeza juhudi zinazofanywa na shirika hilo kwani linaunga mkono juhudi za serikali za kujenga mazingira mazuri ya elimu mkoani Kagera na hivyo kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
“Juhudi hizi hazina budi kuungwa mkono. Huu ni mfano mzuri wa namna wadau wa maendeleo wanavyoweza kuleta tofauti chanya katika jamii. Tutaendelea kufanya kazi pamoja kwa faida ya watoto wetu,” alisema mgeni rasmi.
Bonanza hilo la michezo lililenga kuwafundisha wanafunzi stadi za maisha kama mawasiliano, ushirikiano, utatuzi wa matatizo, usafi binafsi na mazingira, hedhi na hedhi salama.
Afisa Mawasiliano wa shirika hilo, Bw. Lameck Kiula aliwaambia waandishi wa habari kuwa shule hizo saba zilizoshinda katika ngazi ya wilaya zitafaidika na miradi kutokana na mahitaji ya shule husika. Kila shule itapata kiasi cha Tshs Milioni 44 hadi Tshs Milioni 46 kutekeleza miradi tofauti kama madarasa, matenki ya maji, vyoo, vyumba maalum vya hedhi salama, na taulo za kike.
“Lengo ni kuwa na elimu na afya bora na usawa wa kijinsia,” alisema Kiula.
Jambo for Development imejikita katika kuboresha elimu, afya na usawa wa kijinsia mkoani Kagera kwa kutumia mbinu ya michezo ili kuwaunganisha wadau mbalimbali kutekeleza malengo hayo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment