TAKUKURU PWANI YAMULIKA UDANGANYIFU VYAMA VYA AMCOS | Tarimo Blog

Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani, Christopher Myava akizungumza na waandishi wa Habari hawapo pichani leo kwenye ukumbi wa mikutano uliopo ofisini kwake

Na Khadija Kalili
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani leo Machi 28, 2023 wametoa taarifa kwa kipindi cha robo ya Oktoba hadi Desemba mwaka 2022 ambayo imebaini madudu na udanganyifu kwenye Vyama vya Ushirika na Vyama vya Msingi vya Mazao na Masoko (AMCOS).

Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Pwani Christopher Myava amesema kuwa (TAKUKURU) wamefanya kazi ya ufuatiliaji wa miradi 75 ya maendeleo yenye thamani ya Mil.11,421,038,710.71 katika sekta ya Elimu, Afya, Maji na Barabara ambapo wamebaini kuna upungufu kwenye utekelezaji wa Mradi wa  Shule ya Sekondari Viziwaziwa iliyopo Wilayani Kibaha Mjini wenye thamani ya Mil.470 (470,000,000) kwa kuwa na mabati yaliyotumika kuezekea jengo la Utawala,  Maabara na Vyoo vya Shule hayakuwa na kiwango kilichothibitishwa kuezekea majengo ya serikali ambayo ni geji 28 badala yake yalitumika mabati ya geji 30.

"TAKUKURU tumeanza kufanya uchunguzi na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wote waliohusika baada ya uchunguzi kukamilika." Amesema Kamanda Myava

Kamanda Myava amesema kuwa ukarabati wa Skimu ya maji Kijiji cha Mkongo Wilayani Rufiji yenye thamani Mil.500 (512,208,249.03),imebainika katika tanki moja la kuhifadhia maji linavujisha pia milango ya jengo la Ofisi ya Jumuiya ya watumiaji maji Kijiji TAKUKURU na Ofisi ya Meneja wa Mamlaka ya Usambazaji maji vijijini (RUWASA) wamekubaliana kuwa RUWASA wahakikishe mkandarasi anarekebisha mapungufu yaliyobainika kabla ya muda wa matazamio kuisha. 

Akizungumzia kuhusu uchambuzi wa mifumo amesema kuwa ili kudhibiti mianya ya rushwa katika Idara za Serikali na sekta binafsi chambuzi za mifumo tatu zimefanyika kwenye maeneo ya uendeshaji na usimamizi wa masoko ya biashara pamoja na utekelezaji miradi kwa kutumia 'force account' katika Vyama vya Ushirika vya msingi vya mazao na masoko (AMCOS) vya Mkongo Kilimani, Kitupa, Nyaminywili, Kipo na Ngorongo AMCOS zote za Wilayani Rufiji Mkoani Pwani.

Amesema kuwa katika uchambuzi huo wamebaini kuwepo kwa udhaifu katika utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu za Vyama vya Ushirika ambapo baadhi ya nyaraka zimekuwa zikitunzwa nyumbani kwa viongozi wa bodi huku akiitaja AMCOS ya Kipo kuwa baadhii ya nyaraka zake zimeonekaba kuharibiwa na mchwa.

"Hatua hii ya kukosa kumbukumbu ya nyaraka zilizoharibika imesababisha changamoto katika kubaini mapato na matumizi, takwimu na taarifa zote za fedha kwa ujumla. " Amesema Kamanda huyo.

Aidha ameweka wazi kuwa maazimio yaliyowekwa ni kuwa ujenzi wa Ofisi bora ya kutunza nyaraka na kumbukumbu za Ushirika uwe umekamilika ifikapo mwaka 2024.

Kuandaa taarifa za fedha na kujaza taarifa sahihi katika nyaraka zote za Ushirika na kuhakikisha zinatunzwa vizuri ikiwa ni pamoja na kununua bomba la kupulizia dawa za wadudu waharibifu.

"TAKUKURU tumebaini kuwa upo udanganyifu wa kutoandika idadi ya kilo sahihi kulingana na mzigo wa mkulima wakati wa upimaji kwa kisingizio cha ubora na unyaufu, mfano mwananchi anafika na kilo 30.5 lakini kwa makusudi ya kufanya udanganyifu wapimaji ambao ni wajumbe wa Bodi ya AMCOS husika wanamwambia mkulima mazao yako hayana ubora hivyo badala ya kilo 30.5 tutakuandikia kilo 29.

"Hali hii ikiendelea kwa wakulima zaidi wajumbe hao watajikusanyia kilo nyingi kwa udanganyifu nakutengeneza mauzo kwa majina hewa kwa manufaa yao, wananchi wanapogundua udanganyifu huu huacha kuuza mazao kwenye AMCOS zao na kwenda kuuza AMCOS za Kata jirani jambo ambalo AMCOS mama zinakosa mapato lakini pia wananchi wanalazimika kutafuta huduma hii.

"TAKUKURU tumechukua  hatua za kuwataka  kuongeza matumizi ya mizani ya kidigitali na kupunguza matumizi ya mizani ya kusogeza, pia mazao yenye ubora  yasichanganywe ili wakulima wapate madaraja  stahiki." Amesema Kamanda  Myava

Ameongeza kwa kusema kuwa wametoa maelekezo ya kuandaliwe  daftari rasmi  la mapokezi ambalo  wajumbe  wa Bodi  watakuwa wakilihakiki na kusaini kila tarehe ya mapokezo ya mazao.

Imebainika kuwa  AMCOS ya  Mkongo ya Rufiji  kutotoa stakabadhi  kwa wakulima  mara  baada ya kupokea mzigo  baadaye wakulima  hupewa stakabadhi zilizoandikwa kiasi  cha kilo  yofauti na kile  kilichoandikwa awali  wakati  wa kupokea  mzigo  hali hii hutengeneza mianya ya rushwa kwa hao  wajumbe wa bodi  wasio  waaminifu wanaopima mazao  kutoka kwenye kilo zile  walizowapunja  wakulima na kutengeneza  mauzo kwa faida  yao hivyo kusababisha hasara  kwa Ushirika na wakulima.

"Tumebaini kuwa matumizi ya skabadhi  za kuandika na mkono  badala ya POS kukusanyia  ushuru ambazo pia wakati  mwingine hazitolewi  baada ya  malipo kufanywa mfano soko kuu la Mji wa Utete, soko la Kijiji Ikwiriri ukusanyaji wa mapato  bila kutoa skakabadhi  ya mashine POS kwa kisingizio  cha ubovu  wa mashine  hali inayosababisha  upotevu  wa mapato yanayokusanywa ikiwemo soko la Mnarani Wilayani Kibaha  wafanyabiashara waliohojiwa baadhi wamedai kutopatiwa  skakabadhi za malipo kutoka kwa wakusanya ushuru.

Hivyo basi  tumeagiza  kuongeza ufanisi wa matumizi ya POS katika kukusanya ushuru ili kuongeza mapato,ikiwemo kufanha  ukaguzi  wa mara  kwa mara  ili kuongez usimamizi kwa wakusanya  ushuru kwa lengo la kudhibiti.ukusanyaji mapato.

Mwisho Kamanda Myava ametoa wito  wa TAKUKURU kwa wananchi  na wadau wote katika Taasisi za serikali  na sekta binafsi  kuunga  mkono  program  ya TAKUKURU RAFIKI kwani inahusisha  jitihada  za kutambua  na kutatua kero zinazoweza kusababisha  uwepo  wa vitendo  vya rushwa  kama zitaachwa bila kushughulikiwa kwenye sekta  za maji, elimu, nishati (Umeme), afya, barabara, ardhi, huduma za jamii na miradi ya maendeleo inayotekelezwa ba serikali, utatuzi wa kero zitakazoibuliwa kupitia programu hii unatarajjwa kuimarisha  utoaji huduma, kuboresha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuimarisha uzingatiaji wa misingi ya utawala bora na kupunguza vitendo vya rushwa.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2