Na Woinde Shizza, michuzi tv Arusha
WAFANYABIASHARA wa Dawa na Vifaa Tiba Kanda ya Kaskazini wamehimizwa kufuata Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura 219 katika kufanya biashara zao kwa lengo la kuwapatia wananchi bidhaa ambazo ni bora, salama na zenye ufanisi unaotakiwa.
Hayo yamesemwa jana na Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Kaskazini Proches Patrick wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, alisema kumekuwepo na baadhi ya wafanya biashara wasio waaminifu ambao wanakiuka matakwa ya Sheria hiyo kwa kuingiza bidhaa bila kuwa na vibali na wengine kutunza bidhaa ambazo muda wake wa matumizi umepita.
“Bidhaa tunazosimamia ambazo zinatumika hapa nchini ni lazima ubora, usalama na ufanisi wake uwe umehakikiwa na TMDA ili kulinda afya ya wananchi ambao ndio watumiaji wa bidhaa hizo ikiwa ni pamoja na mifugo yetu. Tunafanya ukaguzi wa bidhaa hizo katika vituo vya forodha vya Namanga, Holili, Tarakea na kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro lengo likiwa ni kuhakiki ubora wa bidhaa hizo kabla hazijaingia nchini ili kulinda afya ya jamii, alisema Patrick.
Alisema hairuhusiwi kuingiza dawa au vifaa tiba nchini bila kuwa na kibali cha Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ambapo alifafanua kuwa mfanyabiashara anayetaka kuomba kibali atatumia mfumo wa kieletroniki ambapo pindi anapoomba kibali hicho hupata majibu kupitia mfumo huo na kibali pia atakipata kupitia mfumo huo.
“Tunapenda kuwakumbusha wafanyabiashara kuomba vibali kabla ya kutuma mizigo na sisi tutayafanyia kazi maombi hayo kwa haraka na kutoa kibali baada ya kuhakiki usajili wa bidhaa hizo na kwamba zimekidhi vigezo vya ubora, usalama na ufanisi. Mfumo wetu wa kieletroniki haumlazimishi mteja kuja kwenye ofisi zetu bali tutamwezesha ili aweze kuingia kwenye mfumo wetu na kutuma maombi yake ambapo sisi tutayaona na wakati huo huo kuanza kuyafanyia kazi.” Alisema Patrick
Alisema wao kama TMDA Kanda ya Kaskazini wanasimamia ubora, usalama na ufanisi katika Halmashauri 21 zilizopo katika Mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro na hivi karibuni walikamata na kuzuia bidhaa ambazo hazikuwa na vibali.
Amewataka wafanyabiashara kutumia mipaka iliyo rasmi kuingiza bidhaa zao na kuwaomba wananchi hususani wale wanaoishi maeneo ya mipakani kutoa taarifa TMDA na kwenye vyombo vya usalama endapo watabaini uingizaji wa bidhaa hizo katika mipaka isiyo rasmi (njia za panya).
Alisema licha ya kufanya ukaguzi wa bidhaa hizo zinapoingia hapa nchini lakini pia wanafanya ukaguzi katika maduka na maeneo yote yanayouza, yanayosambaza na yanayotunza bidhaa hizo na kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara ili kuhakiki ubora, usalama na ufanisi wake ikiwa ni pamoja na kuhakiki utunzaji na uwekaji kumbukumbu za usambazaji wa bidhaa hizo.
Aliwakumbusha pia wauzaji wa bidhaa hizo kuhakikisha kuwa zinatunzwa vizuri kwani bidhaa inaweza kuzalishwa vizuri na kuingia nchini ikiwa salama lakini ikaharibika kutokana na utunzaji katika mazingira yasiyokubalika mfano kuhifadhi bidhaa katika mazingira yenye unyevu unyevu na joto kali.
Niwakumbushe pia wauzaji wa bidhaa hizi kuzingatia ukomo wa muda wa matumizi wa bidhaa ,Kuna baadhi ya wafanyabiashara wanatunza na wengine hata kuuza bidhaa zilizoisha muda wa matumizi, hili ni kosa na ni kinyume na matakwa ya Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura, 219.
Alisema kuwa wanafanya kaguzi za mara kwa mara na wanachukua hatua za kisheria kwa wale wote wanaokiuka Sheria lengo likiwa ni kulinda afya ya jamii na afya ya mwananchi mmoja mmoja.
Kaimu meneja wamamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) kanda ya kaskazini Proches Patrick akionyesha waandishi wa habari Jana ofisini kwakwe zilizopo Ndani ya halmashauri ya jiji la Arusha Mahabara hamishika ya kupika ubora, ufanisi ( minilab kit) kama dawa au vifaa tiba vinafaa kutumika kwa binadamu ambapo alibainisha kuwa maabara hii inawezo wa kwenda sehemu yeyote kupima dawa au vifaa tiba.
Kaimu Meneja mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) kanda ya kaskazini Proches Patrick akizungumza na waandishi wa habari Jana katika ofisi zake zilizopo Ndani ya halmashauri ya jiji la Arusha ambapo aliwataka wafanyabiashara wa madawa kufuata Sheria ya dawa na vifaa tiba sura ya 219 pamoja hairusiwi kuingiza dawa au vifaa tiba bila kuwa na vibali vya mamlaka ya dawa na vifaa tiba ambapo wafanya biashara wanaweza kuomba kibali hicho kupitia mfumo wa kieletroniki
(picha na Woinde Shizza).
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment