Kiongozi wa kikosi kazi cha Wizara ya Ardhi cha kumaliza changamoto za urasimishaji Praygod Shao (aliye inama) akitoa elimu kwa wananchi wa mtaa wa Olasiti Kati, Kata ya Olasiti Mkoani Arusha kuhusu uwekaji wa alama za upimaji na utunzaji wake.
Wataalam kutoka kikosi kazi cha Wizara ya Ardhi cha kumaliza changamoto za urasimishaji wakisoma ramani ya upimaji ya mtaa wa Olasiti Kati kabla ya kwenda kukagua alama hizo za upimaji uwandani.
======= ====== =======
Kikwazo kikubwa kinachosababisha kazi nyingi za urasimishaji kukwama na kutokukamilika kwa wakati kimetajwa kuwa ni ukosefu wa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu zoezi zima la urasimishaji. Hayo yamebainishwa mkoani Arusha na kiongozi wa kikosi maalum cha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Praygod Shao kinachofanya kazi ya kutatua changamoto za urasimishaji.
Kiongozi huyo wa kikosi kazi cha Wizara ya Ardhi cha kukwamua kazi za urasimishaji zilizokwama mkoani Arusha, amesema katika ukaguzi aliofanya kwenye eneo la urasimishaji mtaa wa Olasiti Kati uliopo Kata ya Olasiti wananchi wengi wanaonekana hawajui nini maana ya urasimishaji na kwa nini urasimishaji unafanyika katika maeneo yao.
Aidha, kiongozi huyo aliongeza kwamba mtaa wa Olasiti Kati ni moja kati ya mitaa ambayo haina makazi holela ya kutisha ukilinganisha na mitaa mingine ya jiji la Arusha. Hivyo kama wananchi wakipewa elimu ya kutosha kuhusu urasimishaji na wakashirikiana kurasimisha makazi yao watakuwa na mtaa mzuri sana.
‘Lengo la Serikali kuruhusu urasimishaji ni kumhakikishia mwananchi usalama wa milki yake, kumfanya anufaike na kipande cha ardhi anachomiliki pamoja na hakika ya upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii, alisema Praygod’ Nao baadhi ya wananchi wa mtaa wa Olasiti Kati wamesema, walikuwa wanaogopa kushiriki katika zoezi linaloendelea sasa la kurasimisha makazi yao kwa sababu walikuwa hawajui kwa nini warasimishiwe wakati wao ni wazawa wa maeneo hayo na wengine ni maeneo ya babu zao.
Hata hivyo bibi Emma Lodigadi mkazi wa mtaa huo wa Olasiti Kati amesema, yeye alishiriki katika zoezi la awali la kuwatambua wakazi wote wa mtaa wa Olasiti Kati lakini akaogopa kuchangia gharama za kupimiwa na kuwekewa alama za upimaji katika eneo lake. Bibi Emma ameongeza kwamba, sasa hivi ana uhakika kwamba kinachofanyika ni
halali na kina faida kwake kwa hiyo atalipia gharama alizoambiwa na mrasimishaji ili na yeye anufaike na zoezi hilo.
Kwa upande mwingine, mzee John Sharika mmoja kati ya wakazi wa Olasiti Kati ambaye tayari ameshapimiwa eneo lake na kuwekewa alama za upimaji, ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Ardhi kwa kuwapa nafasi hadi watu wa hali ya chini kumiliki kipande cha Ardhi kisheria.
‘Sikuwahi kufikiria kwamba ipo siku na mimi nitapewa hatimilki ya eneo langu kwa hiyo naishukuru sana Wizara ya Ardhi kwa zoezi hili la urasimishaji. Nimeshapimiwa tayari, mipaka yangu iko wazi na alama zangu za upimaji zipo nasubiri kupata hati tuu, alisema mzee John.’
Katika kuhakikisha zoezi la urasimishaji linafikia ukomo na matokeo yanapatikana, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za urasimishaji. Kikosi kazi hicho kimeanza kazi kuanzia Agosti 17, 2020 na hadi kufikia Agosti 30 mwaka huu 2020 kazi zote za urasimishaji zinatakiwa ziwe zimekamilika.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment