LUKA AMUOMBA MAJALIWA HOSPITALI TEULE | Tarimo Blog


MGOMBEA udiwani wa Kata ya Endiamtu, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Chimbason Zacharia amemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kukiangalia kwa jicho la huruma kituo cha afya Mirerani na kukifanya kuwa hospitali teule kwani kinahudumia wagonjwa wa kata zaidi ya sita.

Luka akizungumza kwenye ufunguzi wa kampeni ya CCM katika viwanja vya getini Songambele getini mji mdogo wa Mirerani katika anasema kituo hicho cha afya kimezidiwa. 

Anasema kituo hicho cha afya kinahudumua wananchi wa mji mdogo wa Mirerani na kata za Naisinyai, Shambarai, Mbuguni, Makiba na Majengo. 

Anasema dawa zinazofikishwa kwenye kituo hicho cha afya hazikidhi mahitaji kwani ni kidogo tofauti na idadi kubwa ya watu wanaopatiwa matibabu pindi wakiugua. 

"Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa, pamoja na wananchi wa kata hizo bado wachimbaji madini ya Tanzanite wanapatiwa huduma za afya katika kituo hicho hivyo kiongezewe nguvu," anasema Luka. 

Anasema kituo hicho cha afya Mirerani kina eneo la ekari 15 ya kuweka majengo hivyo kikipatiwa hadhi ya kuwa hospitali teule kinaweza kukidhi haja ya wananchi wa watakaopatiwa huduma ya matibabu. 

"Kutoka Mirerani hadi Orkesumet kwenye hospitali ya wilaya ya Simanjiro ni kilomita 122 na kwenda hospitali ya KCMC mjini Moshi au hospitali ya rufaa ya Mount Meru jijini Arusha ni kilomita 80," anasema Luka. 

Amemshukuru na kumpongeza Rais John Magufuli kwa kukipatia kituo hicho cha afya gari la kubeba wagonjwa ambalo kwa namna moja au nyingine kinasaidia wagonjwa wanaopewa rufaa. 

Hata hivyo, Waziri Mkuu Majaliwa amemuagiza Mkuu wa mkoa huo Joseph Mkirikiti kufuatilia hilo la hospitali teule na kutia mkazo suala la dawa hilo kwani serikali ya awamu ya tano imeongeza bajeti ya dawa kwa hiyo zinapaswa kuwepo. 

Amewataka wananchi wa eneo hilo kumchagua mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Magufuli ili aweze kutimiza matarajio yao kwani mambo mengi ametekeleza katika miaka mitano ya awali. 

Mgombea ubunge wa jimbo la Simanjiro, Christpher Ole Sendeka amewaomba wananchi wa mji mdogo wa Mirerani kuungana ili kuhakikisha Zacharia anashinda udiwani. 

Anasema baada ya mgombea udiwani wa CCM kata ya Mirerani Salome Nelson kupita bila kupingwa ni wakati wa kuungana na kata ya Endiamtu ili kumnadi Luka naye ashike nafasi hiyo. 

"Ndugu zangu tuachane na siasa tufanye maendeleo sasa kwa kuchagua diwani wa CCM, mimi mbunge wa CCM na Rais Magufuli ili tuweze kuimba wimbo mmoja," anasema Ole Sendeka.
 
Mgombea udiwani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Endiamtu Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Zacharia akijinaji kwa wananchi wakati akiomba kura kwenye ufunguzi wa kampeni uliofanywa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2