MMOJA MBARONI KWA TUHUMA YA MAUAJI | Tarimo Blog

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia BARIKI KAJUNI  wa miaka 32 Mkazi wa Makambako, Mkoa wa Njombe kwa tuhuma za kosa la mauaji ya ANSALEMO STAWI @ KISHERIA.

Ni kwamba mnamo tarehe 19.09.2019 majira ya saa 06:00 asubuhi ANSALEMO STAWI @ KISHERIA alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa Zahanati ya Isangawana kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa kukatwa vitu vyenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake na mtuhumiwa BARIKI KAJUNI [32].

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya liliendelea na msako na mnamo tarehe 10.09.2020 majira ya saa 17:30 jioni huko Kitongoji na Kijiji cha Mgololo Mufindi, Wilaya ya Mafinga, Mkoa wa Iringa askari Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na askari wa Mafinga walimkamata mtuhumiwa. Upelelezi unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA MATUKIO YA WIZI WA PIKIPIKI NA UVUNJAJI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia JAMES MWAKABOKO [27] Mkazi wa Forest mpya Jijini Mbeya na BAHATI GELSONI [22] Mkazi wa Ubaruku Wilaya ya Mbarali kwa tuhuma za makosa ya uporaji wa Pikipiki na uvunjaji katika maeneo mbalimbali.

Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 10.09.2020 majira ya saa 01:30 usiku huko eneo la Chunya mjini lililopo Kata ya Itewe, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya baada ya askari kupata taarifa za siri na kisha kuweka mtego uliofanikisha kuwakamata watuhumiwa hao ambao ni wahalifu wazoefu wanajihusisha na mtandao wa matukio ya uporaji, wizi wa Pikipiki na uvunjaji katika maeneo ya Chunya na Mabarali na walitoka gerezani kwa rufaa baada ya kufungwa jela miaka 30 mwaka 2017 Wilaya ya Chunya. Upelelezi unaendelea ikiwa ni pamoja na mahojiano kuhusu matukio waliyofanya pamoja na washirika wenzao.

KUKAMATA SILAHA – BASTOLA NA RISASI ZAKE 07.
Mnamo tarehe 10.09.2020 majira ya saa 20:30 usiku huko Kijiji na Kata ya Isoko, Tarafa ya Kiwanja, Wilaya ya Chunya, Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya baada ya kupata taarifa za siri lilifanikiwa kukamata silaha bastola aina ya Ram maker namba 542909 mali ya SAMOLA LAMEKI KIBALE [56] mfanyabiashara na mkazi wa Isoko.

Aidha silaha hiyo ilikutwa na risasi 07 ndani ya magazine. Silaha hiyo iliibiwa kwenye gari la mhanga huko maeneo ya Kastela - Soweto Jijini Mbeya tarehe 28.04.2020 majira ya saa 23:00 usiku. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako dhidi ya mtu/watu waliohusika katika tukio la wizi wa silaha hiyo.

KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI 
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia TATU FRANK @ NDUMBULA [38] Mkazi wa Lualaje akiwa na nyara za serikali vipande 27 vya mnyama Nyati.

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 14.09.2020 majira ya saa 09:00 asubuhi huko Kitongoji cha Itete, Kijiji na Kata ya Lualaje, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Mkoa wa Mbeya. Mtuhumiwa alikutwa na nyara hizo ndani ya nyumba yake na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

KUPATIKANA NA DAWA ZA KULEVYA – BHANGI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia EZEKIEL EMMANUEL [25] Mkazi wa Mwanjelwa Jijini akiwa na dawa za kulevya aina ya Bhangi gramu 340.

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 14.09.2020 majira ya saa 22:45 usiku huko maeneo ya Mtaa wa Benki, Kata ya Mwanjelwa, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya baada ya kukamatwa na kupekuliwa kwenye nguo alizokuwa amevaa na kukutwa na dawa hizo. Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Imetolewa na:
[ULRICH O. MATEI – SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2