TIMU ya wahandisi kutoka Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), wakifuatilia maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa KM 3.2 linalojengwa mkoani Mwanza kutoka kwa kaimu meneja mradi huo Eng. Abdulkarim Majuto hayupo pichani.
Muonekano wa mtambo wa kuchanganya zege itakayotumika katika ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa KM 3.2 linalojengwa mkoani Mwanza.
Kazi ya ujenzi wa daraja la muda litakalotumika katika kuwezesha kupitisha vifaa wakati wa kujenga daraja la kudumu la Kigongo-Busisi lenye urefu wa KM 3.2 ikiendelea.
Msajili wa wahandisi nchini Eng. Patrick Barozi akisisitiza jambo kwa wahandisi waliopata fursa katika mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa KM 3.2 kujifunza kikamilifu ili kupata ujuzi wa kutosha katika ujenzi huo.
*****************************************
Msajili wa Wahandisi nchini Eng. Patrick Barozi amesema Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), itaendelea kusambaza wahandisi wake katika miradi mikubwa ya ujenzi inayoendelea nchini ili kuwajengea uwezo na uzoefu wa kuisimamia miradi hiyo itakapokamilika.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi lenye urefu wa KM 3,2 na barabara unganishi zenye urefu wa km 1.66 Eng. Barozi amesisitiza umuhimu wa wahandisi wanaopata fursa katika ujenzi wa miradi mikubwa na yakimkakati hapa nchini kujitahidi kuwa na bidii na nidhamu ili kupata ujuzi zaidi utakaorithishwa kwa vizazi vijavyo.
“Fahamuni ninyi ni mabalozi wetu kwenye miradi hii hivyo bidii yenu itawawezesha kujifunza mengi na hivyo kuiwezesha nchi kumudu kujenga miradi kama hii hapo baadae”, amesisitiza Eng. Barozi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi linakojengwa daraja hilo Bw, Juma Sweda amewataka wakazi wa wilaya hiyo kutumia fursa hiyo kufanya biashara na kupata ajira ili kukuza uchumi wao.
Amesema kuwepo kwa ujenzi huo wa miaka minne kukitumiwa vizuri na wananchi kutawapa ajira na biashara nzuri hivyo ni wakati wao kuchangamkia fursa hiyo.
Kaimu meneja mradi huo Eng. Abdulkarim Majuto amesema wamejipanga kuhakikisha watanzania wanapata fursa za ujuzi na waliopata ajira wanalipwa maslahi bora ili daraja hilo liendelee kuleta neema kwa wananchi.
Daraja la Kigogo-Busisi lenye urefu wa KM 3.2 linalojengwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na China Railway 15 Bureau Group Corporation zote za China linaelezwa kuwa la sita kwa urefu barani Afrika na linatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 669 litakapokamilika.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment