ZAIDI YA MILIONI 200 ZATOLEWA NA SERIKALI KUJENGA MAABARA | Tarimo Blog



 Mkuu wa wilaya ya Karatu  Abbas Kayanda akizungumza
na walimu wakuu, Maafisa watendaji wa vijiji, Kata na watumishi wa
Afya katika Tarafa ya Mbulumbulu katika mkutano uliofanyika shule ya
sekondari Diego Wilayani Karatu. 


Na Woinde Shizza ,ARUSHA

SERIKALI imetoa takribani million 210 kwa ajili ya ujenzi wa maabara
katika shule za sekondari wilayani Karatu, Fedha zilizotoka  katika
mfuko wa EP4R, ambapo maabara hizo zitajengwa  katika shule za
sekondari za Domel, Mang’ola, Qurus, Getamock, Baray Khusumay, Diego na
Kansay sekondari.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa wilaya ya Karatu  Abbas Kayanda alipokuwa
akizungumza na walimu wakuu, Maafisa watendaji wa vijiji, Kata na
watumishi wa Afya katika tarafa ya Mbulumbulu  kikao ambacho
alisikiliza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo watumishi  hao
katika maeneo  ya  kazi  na kusema, Serikali itaendelea kuimarisha
miundo mbinu ya afya na elimu hatua kwa hatua.

Kayanda amesema, ujenzi wa maabara hizo ni katika kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini, na katika kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu, bado Serikali inaendelea kuajiri walimu, na pia Halmashauri itagawa walimu
waliopo katika shule ambazo hazina walimu kabisa, mathalani kama shule
ina walimu wa Hesabu au Fizikia wawili basi mmoja aende shule isiyo
na mwalimu hata mmoja wa masomo hayo.

Amesema upo umuhimu wa kuwapongeza walimu wanaofanya vizuri katika
ufundishaji na ufaulishaji, jambo hilo litawaongezea ari walimu katika
kutekeleza majukumu yao ya kila siku.a


Aidha ametoa maelekezo kwa   Maafisa watendaji wa kijiji; kata, na
tarafa kujenga tabia kutembelea taasisi zinazowazunguka katika maeneo
yao ya kiutendaji, ili kubaini changamoto na kuzitatua ikiwa ni pamoja
na kuzitolea taarifa wilayani changamoto ambazo ziko  nje ya uwezo wao
ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Amesema watendaji wanapaswa kufuatilia na kuchukua hatua za kisheria
kwa wanafunzi waliopewa mimba, Maafisa hao watendaji wanapaswa
kufuatilia na kuchukua hatua kwa wanafunzi watoro kwa kuhakikisha
wanarejea shuleni.

Kayanda amesema serikali imefanya ukarabati na ujenzi wa   miundo
mbinu katika kituo cha afya Kambi ya Simba kwa gharama ya zaidi ya
million 500 pia  serikali imepeleka vifaa na  vifaa tiba katika kituo
cha afya kambi ya Simba vyenye thamani ya zaidi ya million 200  na
sasa upo mkakati wa kuchimba kisima cha maji  ili kusaidia kituo cha
afya kambi ya Simba kuwa na maji ya uhakika muda wote.


Ameongeza kuwa   serikali imetoa fedha million 400 Kituo cha afya
Endabash kwa ajili ya ujenzi na ukarabati na ujenzi, kituo hicho cha
afya pia kimepokea vifaa na vifaa tiba, na amewaomba watumishi kuthamini na kutunza miundo mbinu inayojengwa katika sekta ya afya na elimu.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2