* Walia ununuzi gari VXR milioni 470, Ukarabati ofisi na Nyumba
* Wataka uchunguzi maalum matumizi ya rasimali watu na Fedha
Na Woinde Shizza, Michuzi TV Dodoma
KAULI ya Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, kuzitaka Halmashauri
zilizonunua mashangingi ya bei mbaya mkoani Mwanza, kujieleza,
imeendelea kuungwa mkono.
Baadhi ya madiwani wa Manispaa ya Temeke Jijini Dar es Salaam,
wameibua madai mazito wakidai sheria ya manunuzi ya umma
haikuzingatiwa wakati wa ununuzi wa gari la Mkurugenzi wao.
Badala yake, madiwani hao wanamlalamikia Mkurugenzi huyo Lusubilo
Mwakabibi, wakidai alitumia ubabe kuilazimisha kamati ya zabuni
kutekeleza matakwa yake.
Gari lililonunuliwa na manispaa hiyo ni Toyota Landcruser VXR, kwa bei
ya milioni 470, huku wadau wa maendeleo wakidai manispaa inakabiliwa
na changamoto nyingi za kijamii.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa vyumba vya madarasa kwa shuole za msingi, Sekondari pamoja na kukosekana ama ukamilishwaji wa vituo vya afya.
Madiwani hao walidai japo matatizo ya kijamii Temeke yasingemalizwa na
milioni 470 zilizotumika, lakini zingesaidia kupunguza adha za kijamii
katika Manispaa hiyo kongwe.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alipotakiwa kutolea ufafanuzi suala hilo,
hakutaka kulizungumzia kwa kina, badala yake alikiri kuwa ni kweli
wamenunua gari hilo.
“Ni kweli, tumenunua gari hilo, lakini sina majibu kuhusu hilo, mimi
ni mtumishi, kuna mamlaka zinazoweza kutoa majibu kwa niaba yangu
kuhiusu suala hilo, asante.” alisema Mwakabibi.
Mbali na ununuzi wa gari, pia wamedai kuna ubabe unaotekelezwa na
Mkurugenzi huyo kwa watumishi wa idara ya mbalimbali ikiwano ile ya
zabuni na manunuzi, matumizi ya ovyo ya fedha za Umma kwa ajili ya
ukarabati wa ofisi yake na thamani za ofisi hiyo.
Pia walidai fedha zinatumika bila kuidhinishwa na kamati ya Fedha, kwa
ajili ya kazi zikiwemo ukarabati wa nyumba na ununuzi wa thamani za
ofisi na nyumbani kwa mkurugenzi zikiwamo TV kubwa.
“Kuna kamati iliyokuja kuchunguza mambo kadhaa Temeke, kamati ile kwa
hakika haikufanya kazi, badala yake imeacha majeraha kwa watumishi
waliohojiwa.” aliongeza kusema diwani mwingine.
Madiwani hao wamemuomba Waziri Mkuu, kuchukulia hatua kali dhidi ya
mambo yaliyotekelezwa na Mkurugenzi huyo na wengine aliosaidiana nao,
ili kuwa fundisho.
Wamesema hawataki kumfundisha kazi Waziri Mkuu, lakini wanashauri,
Mkurugenzi huyo asimamishwe kazi, ili kupisha uchunguzi wa mambo
mbalimbali, likiwamo suala la kudhalilisha watumishi.
Waliongeza kusema kuwa, wapo watumishi waliofikisha madai yao kwa
ngazi za Wilaya, kwa maana ya ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo wakati huo,
DC Felix Lyaniva, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.
“Huyu ndio mkurugernzi wa kwanza Tanzania kutengeneza mahabusu maalumu ya watumishi, yaani mtumishi akichelewa kazini anawekwa mahabusu, ameweka kontena Manispaa kwa ajili hiyo, mtumishi anakaa mahabusumasaa kadhaa.” alisema mmoja wa diwani.
Waziri wa TAMISEMI Sulemani Jaffo, ambaye ndiye mamlaka ya nidhamu ya
wakurugenzi nchini, hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini
madiwani hao walidai kumfikishia barua ya malalamiko.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment