WAKURUGENZI WATAKAOSHINDWA KUKUSANYA NUSU YA MAPATO MATATANI, JAFO ATUMA SALAMU | Tarimo Blog


Waziri Jafo  akiwasalimia watumishi wa halmashauri ya mji wa Njombe pamoja na kutoa maagizo kwa halmashauri.
Baadhi ya watumishi wa halmashauri ya mji wa Njombe wakimsikiliza waziri Jafo alipopita kwa ajili ya kuwasalimia akielekea mkoani Ruvuma.


Na Amiri Kilagalila, Njombe

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa, (TAMISEMI)  Selemani Jafo amewaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri 185 nchini kuhakikisha wanafikisha zaidi ya 50% ya makusanyo ya mapato ifikapo Januari 15,2021

Ametoa agizo hilo wakati akiwasalimia watumishi wa halmashauri ya mji wa Njombe katika ukumbi wa halmashauri hiyo akipita kuelekea  mkoani Ruvuma huku akiwataka watakaoshindwa kufika nusu ya lengo wajitafakari

“Tarehe 15 mwezi wa kwanza nitatoa taarifa ya miezi 6 ya ukusanayaji mapato,wakurugenzi wote wa halmashauri 185 wakajipime wakati wanaenda krismasi sitaki kuona halmashauri yoyote iliyopata chini ya 50%”alisema Waziri Jafo.

Jafo aliongeza kuwa “Halmashauri itakayokuwa imekusanya chini ya 50%  mkurugenzi  huyo je anafaa kuendelea na serikali ya awamu ya pili ya kipindi cha tano cha Dkt,John Pombe Magufuli ama hatoshi awekwe pembezoni aje mwingine anayeweza kukusanya mapato.”aliongeza Jafo.

Amesema, “Hatutashughulika na wakurugenzi peke yake tutashughulika na watunza hazina pamoja na maafisa mipango,hili ni agizo langu kwa halmashauri zote nchi nzima.'' Aliongeza.

Aidha waziri Jafo ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Njombe na mkurugenzi wake  Ally Juma kwa kufanikiwa kuongoza katika taarifa yake iliyoishia jana 21 Disemba ikionyesha Halmashauri hiyo kuongoza kimkoa na kuwa miongozni mwa halmashauri inayofanya vizuri kitaifa.

“Naipongeza halmashauri ya wilaya ya Njombe ambayo mpaka jana tarehe 21 Disember kwenye taarifa yangu wamekusanya bilioni 1.707 sawa na 72%  na ni miongoni mwa halmashauri mpaka leo zilizokuwa kinara Tanzania kwa ukusanyaji wa mapato.”alisema Seleman Jafo

Hata hivyo amesema halmashauri ya Wilaya ya Makete ndiyo inayofanya vibaya mpaka sasa katika mkoa wa Njombe kwa kukusanya milioni 599

“Taarifa yangu mpaka jana inaonyesha halmashauri ya wilaya ya Makete imekusanya milioni 599 sawa na 25%  nje ya bilioni 2.441 kwa hiyo mna kazi kubwa ya madeni.” alisema Jafo.

“Halmsahauri ya mji wa Njombe imekusanya 48% mpaka jana 21 Disemba sawa na 3.299 bilioni tunapomaliza mwezi huu disemba tunatarajia halmashauri zote ziwe zimekusanya sio chini ya 50%.”alisema waziri Jafo

Mbunge wa jimbo la Njombe mjini Mh,Deodatus Mwanyika amemshukuru waziri Jafo kwa kufika katika halmashauri hiyo na kukagua baadhi ya miradi inayojengwa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Njombe.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2