Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, akitoa taarifa kuhusu Muundo na Majukumu ya wizara ya Ujenzi na Uchukuzi aliyouwasilisha mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Wakurugenzi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, wakisikiliza taarifa ya Mheshimiwa Waziri Mhandisi Leonard Chamuriho (hayupo pichani) kuhusu muundo wa Wizara hiyo, jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Suleiman Kakoso, akifafanua jambo kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya Wizara yake kwa kamati hiyo, jijini Dodoma.
*********************************************
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundominu imeiagiza Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha wanakarabati barabara zao ili ziweze kupitika vipindi vyote vya mwaka.
Akizungumza mara baada ya kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika leo jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Suleiman Kakoso, amesema kuwa katika kipindi hiki cha masika miundombinu mingi ya barabaara imekuwa ikiharibika na hivyo ameutaka Wakala huo kujipanga na kukarabati barabara ambazo zina changamoto.
“Tumeshuhudia katika kipindi hiki cha masika ambapo mvua nyingi zinanyesha nchi nzima na kuharibu miundombinu, Kamati inaiagiza TANROADS kujipanga na kuhakikisha inakarabati barabara hizi ziweze kupitika ili wananchi waweze kupata huduma za msingi”, amesema Kakoso.
Aidha Kakoso, amesema kuwa Kamati yake itahakikisha kuwa utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imetoa fedha nyingi inayosimamiwa na Wizara kupitia taasisi zake inafanyika kwa ufansi ili kuweza kuleta maendeleo kwa wananchi.
Amewataka wakandarasi waliopewa dhamana ya kutekeleza miradi inayosimamiwa na Sekta ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha wanaikamilisha kwa wakati ili wananchi kuweza kunufaika nayo.
“Tunajua kabisa bila kuwa na miundombinu huwezi kuwa na maendeleo, tumeshuhudia katika kipindi hiki miundombinu mingi inatekelezwa, tunaamini miundombinu hii ikikamilika maendeleo makubwa yatapatikana nchini”, amesisitiza Kakoso.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, amesema kuwa Wizara kupitia Taasisi zake imejipanga kusimamia na kutekeleza miradi kwa wakati ili kunufaisha wananchi na nchi kwa ujumla.
“Tumekutana na kamati na tumewaeleza mipango yetu ya Wizara pia tutahakikisha tunaisimamia miradi yetu ili iweze kukamilika kwa wakati na kuweza kuchochea maendeleo ya nchi”, amesema Chamuriho.
Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kusimamia utendaji wa taasisi inazozisimamia kwa kuendelea kuzijengea uwezo wa kitaasisi na kuendelea kujenga nidhamu na uadilifu kwa wafanyakazi.
Naye, Mjumbe wa Kamati hii ambaye ni Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Tanga, Mheshimiwa Mwanaisha Lulenge, amefafanua kwa niaba ya wajumbe wenzake watahakikisha wanasimimia na kusimamia Serikali kutatua changamoto zinazokabili Sekta hii.
“Tumejipanga kuhakikisha tunatoa ushauri, tunasimamia kwa karibu utekelezaji wa Serikali kupitia Sekta hii na kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo bora kwa wakati kupitia Sekta hii”, amesisitiza Mheshimiwa Lulenge.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment