*Wasema walioteuliwa na Rais wajue wana deni kubwa
*Wasisitiza wakasimamie ukusanyaji mapato ya Serikali
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MAKAMU wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Philip Mpango amewaambia walioteuliwa na kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika Serikali watambue wamepewa heshima kubwa na Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo hilo ni den ambalo wanatakiwa kulilipa kwa kufanya kazi kwa bidii katika kuwatumikia Watanzania.
Akizungumza leo Aprili 6, mwaka 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam, Dk.Mpango pamoja na mambo mengine amesema anaungana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwapongeza wote walioteuliwa na kula kiapo."Nataka kusisitiza kuteuliwa kwenu ni imani kubwa ambayo mmepewa na Rais, lakini hilo ni deni kubwa kwa Rais na deni kubwa kwa watanzania, ni deni ambalo mnatakiwa kulilipa kuanzia sasa.
"Mnatakiwa kulipa kwa kazi nzuri ambayo imetukuka, nchi yetu bado, tumefikia uchumi wa kati lakini tunatakiwa kuitoa nchi yetu hapa ilipo na kwenda mbele zaidi.Naomba kusisitiza Waziri Mkuu,amewasisitiza kwenda kusimamia ukusanyaji wa maduhuli, mimi nataka kusisitiza upande wa pili kila mmoja weu mkasimamie matumizi adili ya rasilimali za umma mkianza na watumishi wenyewe.
"Ninyi mnatakiwa kuwa makini katika kusimamia rasilimali hizo, lakini pia rasimali fedha mzingatie kanuni na sheria ya matumizi ya fedha za umma, nendeni mkasimamie mafuta ya magari, matengenezo kwenye magari, mkasimamie miradi ya maendeleo kuna udanganyifu mkubwa,"amesema Dk.Mpango.
Ameongeza kwa sasa bajeti ya Serikali inaandaliwa hivyo wakaisimamie ipasavyo huku akionya tabia ya utaratibu wa kila baada ya muda mfupi kuomba uhamisho wa fedha kwani inaonesha bajeti haiandaliwi vizuri."Kwenye hilo Rais nitakusaidia.Pia wanaosimamia Muungano naomba mwende mkasimamie ipasavyo kwa kushirikiana na wenzetu wa Zanzibar, tunataka changamoto zilizopo tuzimalize kabisa, hivyo wale wanaoshughulika na changamoto za Muungano mhakikishe mnazimaliza kabisa".
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka walioteuliwa na kula kiapo kwenda kutekeleza majukumu yao lakini wakasome ,waelewe Wizara zao na majukumu yao ili wakawatumikie Watanzania. "Makatibu Wakuu na Manaibu wanalo jukumu kubwa sana,hakikisheni majukumu ya Wizara ya kila siku yanakwenda vizuri.
"Muwe na mpango kazi ambao unakidhi mahitaji ya Rais, lakini mahitaji ya kuwatumikia Watanzania, hakikisheni kila mwenye dhamana ambaye yuko chini yenu utendaji wao uwe wenye nidhamu wa hali ya juu, tunataka wananchi wasikilizwe na wahudumiwe na ofisi zetu.
"Mbali ya nidhamu tunajukumu kila palipo na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali yakusanywe vizuri ili tutatekeleze miradi, tunataka kuhakikisha miradi yote iliyopo na ile ambayo imeahidiwa lazima itekelezwe. Hivyo kila mmoja ahakikishe miradi inakamilka kabla ya mwaka 2025,kila mtendaji akaangalie miradi iliyopo kwenye wizara yake ili itekelezwe,"amesema Waziri Mkuu.
Aidha amesisitiza wahakikishe uchumi wa nchi yetu uwiano sawa ." Alhamis nitakuwa na kikao kazi na watendaji wote wa taasisi, tutapeana maelekezo ya nini kinatakiwa kufanyika."
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment