RC KUNENGE AIAGIZA HALMASHAURI YA MJI WA KIBAHA KUFUNGA HOJA ZA UKAGUZI IFIKAPO JUNI 30 | Tarimo Blog

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

SERIKALI Mkoani Pwani ,imeiagiza halmashauri ya Mji wa Kibaha ,kuhakikisha inafunga hoja zote 16 ,ambazo hazijafungwa katika ukaguzi wa hesabu za Serikali ,kwa mwaka 2019/2020 ,hadi ifikapo Juni 30/mwaka huu.

Aidha halmashauri hiyo imetakiwa ,kukusanya madai ya fedha ambapo inadai milioni 877.128 ambazo zipo mikononi mwa vikundi vya vijana,wanawake na walemavu ,hivyo ameagiza kuunda timu itakayofuatilia suala hili ili apate taarifa haraka kisha kukamilisha taarifa ya mkaguzi.

Akitoa maagizo hayo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Pwani ,Aboubakar Kunenge ,wakati wa baraza la madiwani kupitia na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali (CAG )mwaka 2019/2020, mkuu wa wilaya ya Kibaha mhandisi Martin Ntemo alisema ,hoja hizo zifungwe na kama watakwama watoe taarifa.

Pamoja na hayo,alieleza ni wakati wa kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi ambao watabainika kusababisha hasara kwa halmashauri.Ntemo aliongeza ,adhabu itakayotolewa ilingane na ukubwa wa hasara aliyosababisha mtumishi lengwa ili kusaidia kulinda maadili na uwajibikaji.

Pia taarifa hiyo ya mkuu wa mkoa, ilielekeza ,kutenga fedha kwa miradi iliyokwama muda mrefu .
"Epukeni kuzalisha hoja ,ongezeni wigo wa ukusanyaji mapato na halmashauri ibuni vyanzo vipya vya mapato ili kuinua mapato ." alisema Ntemo.

Ntemo ,aliongeza ili kutekeleza ilani ya CCM ,madiwani waendelee kusimamia miradi kwa maslahi ya wananchi kwa lengo la kutunza matarajio ya wananchi.Nae mkaguzi mkuu wa hesabu ,Mkoani Pwani Mary Dibogo ,alisema halmashauri hiyo ina madeni makubwa japo ina hati safi .

Aliitaka halmashauri hiyo ,kusimamia ukusanyaji wa mapato ,na kuhakikisha yanafika sehemu sahihi .
Kwa upande wake ,Katibu tawala Mkoani Pwani ,Mwanasha Tumbo alitoa rai kwa watumishi na watendaji kuacha kufanya kazi kwa mazoea .

Mwanasha aliwaasa kufuata sheria ,kanuni na muongozo katika masuala ya ukaguzi ili kuondokana na dosari ndogondogo.Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kibaha ,Jeniffer Omolo alibainisha ,kati ya hoja 38 kufikia juni 2 mwaka huu 22 zilifungwa ambapo hoja 16 hazijafungwa.



 
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2