RAIS Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Samia anatarajiwa kuongoza viongozi wakuu wa nchi, viongozi wa kimataifa na watanzania katika mdahalo maalum wa kumbukizi ya maisha ya aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamin William Mkapa mdahalo utakaofanyika Julai 14 katika ukumbi wa Mlimani City Mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mkoani Dar es Salaam Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya 'Benjamin Mkapa Foundation' Dkt. Ellen Mkondya - Senkoro amesema, Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa kushirikiana na Serikali wameandaa mdahalo huo wa kumbukizi ya maisha ya Hayati Benjamin William Mkapa ikiwa sehemu ya kuenzi mchango wake katika taifa, Afrika na dunia kwa ujumla kwa kauli mbiu ya "Hayati Benjamin Mkapa: Mwaka Mmoja Tangu Atutoke, Tunayakumbuka Maisha Yake, Tunaenzi Urithi Wake."
Amesema, Rais Samia ataongoza mdahalo huo ambapo washiriki kutoka ndani na nje ya nchi wanaotarajiwa kushiriki kupitia uwepo wao binafsi au kwa njia ya mtandao.
"Baadhi ya viongozi mashuhuri wanaotarajiwa kushiriki katika tukio hilo muhimu la kukumbuka maisha ya Mzee Mkapa ni pamoja na aliyekuwa Rais wa 42 wa Marekani Bill Clinton, aliyekuwa Waziri mkuu wa Uingereza Tonny Blair, aliyekuwa Rais wa Nigeria Olegesun Obasanjo na Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI (UNAIDS,) Winnie Byanyima ambao wote kwa pamoja watatoa salamu zao kwa njia ya video wakieleza walivyomfahamu Hayati Benjamin Mkapa katika kushirikiana naye katika kazi na masuala mbalimbali ya kuleta maendeleo duniani hususan katika bara la Afrika na nchini Tanzania." Amesema Dkt. Ellen.
Aidha amesema, viongozi wengine wa kitaifa watakaoshiriki mdahalo huo ni pamoja Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt.Hussein Ally Mwinyi, Marais wastaafu, viongozi wakuu wa nchi kutoka Tanzania Bara na Visiwani, mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini, wakuu wa mashirika ya Kimataifa nchini, wakuu wa Taasisi mbalimbali za Umma na binafsi, wanafamilia na marafiki wa Hayati Benjamin William Mkapa kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na asasi za kiraia, viongozi wa dini na watanzania wote watakaoshuhudia mdahalo huo kupitia vyombo vya habari.
Vilevile amesema, katika mdahalo kutakuwa na mada ya "Afya kwa Wote: Urithi wa Rais Benjamin Mkapa katika Kujenga Mifumo ya Afya Imara na Endelevu." Ambapo washiriki watapata wasaa wa kusikia mjadala jinsi Hayati Benjamin William Mkapa alivyofanikisha mifumo ya afya kwa kuhakikisha kila mtanzania anapata fursa ya kupata huduma za afya.
Aidha amesema, kupitia mdahalo huo Rais Samia atazindua mfuko maalumu wa Taasisi hiyo ilianzishwa na Hayati mkapa miaka 15 iliyopita "Endowment Fund" ambao umeanzishwa na taasisi hiyo katika kuongeza chachu katika kuimarisha huduma za afya nchini.
Hayati Benjamin William Mkapa alifariki dunia Julai 23, 2020 na tukio hilo la mdahalo litafanyika wiki moja kabla ili kutoa nafasi kwa ndugu, jamaa, marafiki na watanzania kwa ujumla kumuenzi kiongozi huyo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment