Na Mwandishi Wetu
TANZANIA na Rwanda zamekubaliana kushirikiana katika kukuza Sekta ya Mawasiliano hasa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili kuongeza tija katika mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Wananchi katika Nchi hizo mbili.
Hayo yamebainika jijini Dar es salaam Tarehe Julai 16, 2021 wakati wa ziara ya Waziri wa Habari na TEHAMA wa Rwanda Bi. Paula Ingabire ambae akiwa ameambatana na mwenyeji wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) walipotembelea Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA, ziara ambayo ilitanguliwa na mkutano wa pamoja kujadili namna nchi hizo mbili zinavyoweza kushirikiana katika kukuza sekta ya mawasiliano.
“Kama mnavyofahamu nchi zetu hizi zina mahusiano ya muda mrefu lakini ni nchi ambazo zote mbili zinapiga hatua kubwa sana katika sekta ya Mawasiliano na TEHAMA; lakini sambamba na hilo ni nchi ambazo zinategemeana katika suala la Mawasiliano” alisisitiza Waziri Ndugulile.
Waziri Ndugulile amebainisha kuwa Tanzania inapeleka mawasiliano katika nchi zote Saba za Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba ushirikiano baina ya Tanzania na Rwanda umekuja muda muafaka kwa kuzingatia kuwa Rwanda inapitisha mawasiliano yake nchini Tanzania.
Tanzania inaendelea na kazi ya kuunganisha huduma za mawasiliano na nchi za Congo DRC na Msumbiji ambazo Waziri Ndugulile amesisitiza ndizo zilizosalia katika ukanda wa nchi zinazoizunguka Tanzania katika kuunganisha mawasiliano.
“Tunataka sisi kama Tanzania kuwa ni kitovu cha Mawasiliano katika Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati” aliongeza Ndugulile.
Katika mkutano huo wa pamoja wa Mawaziri, Tanzania na Rwanda zimekubaliana kubadilishana uzoefu, kubadilishana utaalam na wataalam ambapo kila upande utapata fursa ya kujifunza na kuona fursa tumizi kutoka upande mwingine.
Akizungumzia kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi wote wa Tanzania Waziri Ndugulile amesisitiza kuwa Serikali tayari imefanya uwekezaji mkubwa wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kwamba zaidi Kilomita 8000 za Mkongo wa Taifa zimejengwa na kwamba kazi ya kufikisha huduma za Mkongo kama njia kuu ya mawasiliano inaendelea kutoka ngazi ya mkoa kuelekea wilaya na hatimae kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi wote.
“Tunajenga uwezo na jambo moja ambalo sisi kama Serikali tunalifanya ni kuhakikisha kwamba vifaa vya TEHAMA, ikiwa ni pamoja na simu janja zinapatikana ambapo sasa Serikali imefuta kodi ili sasa simu zishuke bei na wananchi waweze kumudu kununua simu janja” alisisitiza Ndugulile.
Kuhusu mawasiliano katika maeneo ya mpakani mwa nchi, Ndugulile amebainisha kuwa Serikali itahakikisha inafanya uwekezaji kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kwamba tayari Serikali imetangaza Kandarasi ili kutibu tatizo la changamoto ya mawasiliano maeneo ya mipakani.
“Tutakwenda kutumia zaidi ya Shilingi Bilioni 45 kuhakikisha kwamba tunaboresha Mawasiliano pembezoni mwa nchi ili kuhakikisha kwamba, mawasiliano ya simu katika maeneo haya ya pembezoni yanakuwa upande wa Tanzania” alibainisha Waziri Ndugulile.
Ameongeza kuwa Serikali itahakikisha mawasiliano ya redio na simu katika maeneo ya mipakani yanakuwa ya upande wa Tanzania, ili kuepusha wananchi wa Tanzania waishio mipakani kukosa huduma za mawasiliano za ndani na badala yake kupokea huduma hizo kutoka nchi jirani.
Kwa upande wake Waziri wa Habari na TEHAMA wa Rwanda Mhe. Paula Ingabire amesisitiza kuwa Rwanda ina nia ya dhati ya kukuza ushirikiano katika huduma za mawasiliano baina ya nchi hizo mbili na kwamba kwenye mkutano wa pamoja nchi hizo mbili zimekubaliana kutumia TEHAMA kama nyenzo ya kufikia lengo la uchumi wa kidijitali.
“Kwa hivyo hatua ya kuanzia iko ndani ya taasisi zetu katika ngazi ya uundaji wa sera, wizara, wasimamizi, sekta ya utangazaji, huduma za posta na nyingine, tunataka kuimarisha ushirikiano huo wa ki-taasisi, na tumekuwa na uhusiano mzuri na taasisi za Tanzania kama TCRA na TTCL na kwa wizara hii mpya ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Tanzania tunataka kukuza zaidi ushirikiano baina yetu” alibainisha na kuongeza Waziri Ingabire.
Awali kabla ya mkutano na Waandishi wa Habari Mawaziri hao walipokea mawasilisho yanayobainisha namna huduma za mawasiliano zinazosimamiwa na wizara husika zinavyofanya kazi kutoka Taasisi zilizo chini ya wizara zao na kisha kujadiliana kabla ya kutoa taarifa kwa umma; Waziri Ingabire na ujumbe wake walitembelea Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Kituo cha Kuhifadhi Data.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment