USIKIVU WA TBC WAPANDA KWA ASILIMIA 14 NDANI YA MIEZI MIWILI | Tarimo Blog


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Innocent Bashungwa(Mb), na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.Dkt. Faustine Ndungulile (Mb);  wakikata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Kituo cha kurushia matangazo ya Redio ya TBC eneo la Kisaki - Morogoro leo Julai, 2021.
Mtaalam wa Mitambo akitoa maelezo kwa  viongozi  mbalimbali waliohudhuria  kwenye ya uzinduzi wa Kituo cha kurushia matangazo ya Redio ya TBC eneo la Kisaki - Morogoro leo Julai, 2021.

Na John Mapepele, WHUSM
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe Innocent Bashungwa amesema hadi kufikia Mwezi Septemba, mwaka huu usikivu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) utapanda kuzifikia Wilaya 120 sawa na 76% kutoka Wilaya 103 ambapo ni sawa na 64% za usikivu wa sasa ili kuhahakikisha wananchi wote wanapata habari kwa uhakika.

Mhe. Bashungwa ameyasema hayo leo Julai 30, 2021 kwenye uzinduzi wa kituo cha kurushia matangazo ya redio eneo la Kisaki mkoani Morogoro ambapo amesema katika Bajeti ya Maendeleo ya Wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021, TBC inatekeleza miradi ya upanuzi wa usikivu katika Wilaya za Karagwe (Kagera), Same (Kilimanjaro), Sikonge (Tabora), Kahama (Shinyanga), Bunda (Mara), Nkasi (Rukwa) na Kasulu (Kigoma)ambapo amefafanua kuwa kukamilika kwa miradi hii kutawezesha usikivu wa TBC kufikia 76% ya nchi nzima.

“Nataka kuwahakikishia wananchi wote kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi shupavu wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakusudia kupanua usikivu wa redio za TBC nchi nzima” amesisitiza Mhe. Bashungwa

Ameyataja maeneo mengine ambayo miradi inaendelea kutekelezwa kwa ushirikiano wa TBC na UCSAF kuwa ni pamoja na wilaya za Ngara (Kagera), Kyela (Mbeya), Ruangwa (Lindi), Kilombero/Mlimba (Morogoro), Ludewa (Njombe), Tanganyika (Katavi), Makete (Njombe), Uvinza (Kigoma), Mbinga (Ruvuma) na Ngorongoro (Arusha).

Pia ametoa wito kwa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kupeleka miundombinu ya umeme kwa vituo vyote ambavyo vinatumia genereta mfano Karagwe ili kuendelea kupunguza gharama za uendeshaji wa miradi hii.

“Kabla ya mradi kuanza kutekelezwa TBC, TANESCO na UCSAF kaeni pamoja mjadiliane namna ya kutekeleza miradi hii kwa ufanisi ili kutatua shida zinazowakabili wananchi wetu kwa kukosa huduma ya Habari na Mawasiliano” amesisitiza Mhe. Bashungwa

Kwa upande mwingine ameiomba Wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS na TAMISEMI kupitia TARURA waone namna ya kuwezesha kufikika eneo hilo la mradi wa Kisaki kwa urahisi zaidi.

“Ombi hili ni sambamba na maeneo mengine yenye mitambo ya kurusha matangazo ambayo miundombinu yake haiko vizuri mfano eneo la Mnyusi- Tanga, Imagi – Dodoma, Matogoro – Songea na Mlima kampuni – Katavi)”. Ameongeza Mhe. Bashungwa.

Amesema kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (Ibara 125) inaelekeza Serikali kuhakikisha kuwa inawekeza katika uimarishaji wa miundombinu ya utangazaji kwa TBC.

Mhe. Bashungwa amefafanua kuwa kwa namna ya pekee ibara ya 125 (f) inalekeza kuwa Serikali itahakikisha kuwa “inaimarisha Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kwa kulijengea uwezo wa rasilimaliwatu, fedha na vifaa vya kisasa ili liweze kufikisha matangazo ya redio na televisheni nchini kote kwa ubora na usikivu mzuri....”.

Aidha amesema Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka mitano (2020/2021 - 2025/2026) umeainisha vipaumbele vyake katika uwekezaji wa miundombinu ya Utangazaji ya TBC, ikiwemo upanuzi wa usikivu wa redio, pamoja na miundombinu yake.

Ameisihi Menejimenti ya Shirika hilo kuendelea kuwa wabunifu katika kuhabarisha umma na kuwahakikishia kwamba Wizara yake itaendelea kuwapatia msaada wowote wanaohitaji ili kutimiza malengo yake. Amelitaka TBC kuhakikisha linaandaa maudhui yatakayokidhi matakwa ya jamii nzima ya watanzania katika kukuza uzalendo, kudumisha mila na desturi za Watanzania na kulinda tunu za Taifa.

Pia amelipongeza TBC kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwahabarisha wananchi wa makundi yote, ambapo amesema anatambua jitihada zinazofanywa za kukamilisha uzinduzi wa chaneli mpya ya televisheni ya TBC2 itakuwa mahususi kwa ajili ya vipindi vya vijana, michezo na burudani ambayo ujenzi wa studio zake umekamilika Mikocheni, Dar es Salaam.

Amewashukuru wadau wote ambao wanafanikisha utekelezaji wa mradi wa usikivu wa TBC hapa nchini. Amewataja baadhi ya wadau hao kuwa ni pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya jamii,Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kuendelea kufadhili miradi hii ya Upanuzi wa Usikivu ambayo inatarajiwa kutatua changamoto za Usikivu hivyo kuwezesha wananchi kupata huduma ya habari na Mawasiliano kwa urahisi zaidi.

Amesema uzinduzi wa kituo hiki ni hatua muhimu katika kutekeleza malengo Serikali katika kufisha habari kwa wananchi wote, mahala popote kwa lengo la kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha kwa njia ya redio, televisheni na mitandao ya kijamii. TBC kikiwa ni chombo cha Utangazaji cha Umma, kimetekeleza jukumu hili kwa vitendo.


Matangazo ya Redio za TBC kupitia kituo hiki yanatarajiwa kuwafikia wananchi katika vijiji vya Mvuha, Dhutumi, Bwakila Chini, Dakawa, Mngazi, Milengwelengwe, Sesenga, Nyalutanga, Mdokonyole, Gomelo, Kisaki Station, Matambwe, Kolelo, Lukange, Mgata, Ngerengere, Singisa na kwingineko). Maeneo mengine yatakayonufaika na mradi huu ni katika Wilaya za jirani za Kilombero, Rufiji na Kilwa.

“Kuzinduliwa kwa matangazo ya Redio katika kituo hiki cha Kisaki, ni utekelezaji wa Ilani ya CCM (2021 – 2025), ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu kuzinduliwa kwake”.amesisitiza Mhe. Bashungwa.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2