Pesa za TASAF kipindi cha pili awamu ya tatu kulipwa Kidigitali. | Tarimo Blog

Na John Walter-Babati

Serikali ya Tanzania imesema ipo mbioni kuanza kulipa fedha za mpango wa kunusuru kayamaskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kwenda kwa walengwa kwa miamala ya simu, wakala maalum na kupitia kwenye mabenki ili kupunguza gharama na fedha kuwa salama.


Hayo yameelezwa leo Jumanne agosti 10, 2021 na ofisa uwezeshaji na ufuatiliaji wa Tasaf, Salimu Mshana katika kikao cha kuwajengea uelewa viongozi wa Halmashauri ya wilaya Babati na wawezeshaji kuhusu awamu ya pili ya mpango wa tatu wa Tasaf.

Mshana amesema utaratibu huo utasaidia walengwa kujiwekea akiba kuliko kuwa na fedha zote ndani.Ameeleza kuwa tathmini ya utekelezaji wa Kipindi cha kwanza cha awamu ya tatu ya TASAF imeonyesha kwamba mpango huo umechangia katika kufikiwa kwa azma ya serikali ya kupunguza umaskini nchini ambapo takwimu zinaonyesha kuwa umaskini wa mahitaji ya msingi kwa kaya za walengwa umepungua kwa asilimia 10 na umaskini uliokithiri kwa kaya za walengwa umepungua kwa asilimia 12,mafanikio yaliyotokana na walengwa kujikita kwenye shughuli za kukuza kipato na kujiimarisha kiuchumi kwa kufanya shuhguli mbalimbali ikiwemo Kilimo, ufugaji, uvuvi na miradi ya ujasiriamali.

Ikumbukwe kwamba kipindi cha pili cha awamu ya tatu ya TASAF 2020-2023 kinatekelezwa kwenye halmashauri 184 za Tanzania Bara na Unguja na pemba,Zanzibar ambapo kitafikia kaya milioni 1,450,000 zenye jumla ya watu zaidi ya Milioni Saba kote nchini huku wanufaika wakiwa ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaohudhuria kliniki,wanafunzi wa shule za awali,shule za msingi na Sekondari, mama mjamzito na mwanakaya mwenye ulemavu.

Awali akifungua kikao hicho, mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange amewataka wawezeshaji kutoa elimu mara kwa mara ili wanufaika wajue umuhimu wa fedha hizo kwani wakitumia kama malengo yalivyo itasaidia kupunguza umaskini na utegemezi.

Amewataka wanaosimamia mpango huo kuhakikisha walengwa wanaofikiwa ni wale ambao kaya zao haziwezi kumudu au haina uhakika wa kupata Milo mitatu kwa siku kuanzia kifungua kinywa, mlo wa mchana na usiku na inayoishi kwenye makazi duni.

Naye Mwenyekiti wa Halmshauri ya wilaya ya Babati John Noya amesema wameupokea mpango huo na kwamba watasimamia kikamilifu ifike kwa walengwa na kuwanufaisha.Katika mjadala Madiwani wamesema hawana uhakika Kama mfumo wa malipo ya fedha za mradi kwa walengwa kwa njia ya kielekroniki utafanikiwa kwa kuwa halmashauri ya Babati haina mfumo mzuri wa mawasiliano.


 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2