Na. Damian Kunambi, Njombe.
Jeshi la polisi wilayani Ludewa mkoani Njombe limezitaka taasisi zote za mikopo zilizopo wilayani humo kuhakikisha kuwa zina kibali kutoka benki kuu ya Tanzania (BoT) cha kutoa huduma hizo pamoja na leseni kutoka kwa wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA) ili kuendesha shughuli hizo kwa usalama zaidi.
Hayo ameyasema mkuu wa jeshi la polisi wilayani humo Deogratius Masawe alipofanya mkutano na taasisi mbalimbali za utoaji mikopo zilizopo katika wilaya hiyo kwa lengo la kuwakumbusha sheria na taratibu wanazotakiwa kuzifuata katika kutoa huduma hiyo.
Amesema uwepo wa taasisi hizo kiholela kunapelekea kuumiza wananchi wanaoenda kuchukua mikopo hiyo kwani wamekuwa wakilimbikiwa riba zisizo na mpangilio kitu ambacho kinarudisha nyuma uchumi wa wananchi hao.
"Unakuta mtu kaenda kukopa shilingi laki tano lakini mpaka anamaliza deni anajikuta amelipa zaidi ya milioni moja hadi mbili kitu ambacho ni unyanyasaji ambao haukubaliki", Amesema Masawe.
Ameongeza kuwa endapo kampuni hizo zitatambulika kisheria itasaidia kupunguza vitendo kandamizi kwa wateja wanaopata huduma za mikopo.
Aidha ametoa onyo kwa taasisi ambazo zipo kisheria lakini ndani yake kuna uvunjifu wa sheria hizo ambapo hutumia nguvu katika kufuatilia madeni yao ikiwemo kuwanyang'anya wateja wao ATM card pamoja na password zake.
"Kwa kawaida mtu anapochukua mkopo anatakiwa kuweka dhamana ya kitu kinacho uzika, lakini inashangaza kuona hawa wakopeshaji wanachukua ATM kadi za wateja tena na password kitu ambacho hakikubaliki kisheria", Amesema Masawe.
Aidha kwa upande wa baadhi ya wakopeshaji hao wamedai kuwa wanatumia nguvu katika kudai madeni kutokana na wadaiwa wao kukaidi kulipa madeni yao kwa wakati na kuanza kuwasumbua.
Wamesema kwa elimu waliyoipata kutoka kwa mkuu huyo wa jeshi la polisi wameielewa na watajitahidi kufuata utaratibu sahihi katika utoaji huo wa mikopo.
Mkuu wa jeshi la polisi wilayani Ludewa mkoani Njombe Deogratius Masawe (kulia) akipitia baadhi ya nyaraka za usajili za taasisi mbalimbali zinazotoa mikopo wilayani humo.
Mkuu wa jeshi la polisi Wilayani Ludewa Deogratias Masawe akipokea nyaraka za usajili kutoka kwa maofisa mikopo mbalimbali wilayani Ludewa.
Mkuu wa jeshi la polisi Wilayani Ludewa Deogratias Masawe akipokea nyaraka za usajili kutoka kwa maofisa mikopo mbalimbali wilayani Ludewa.
Baadhi ya Maafisa mikopo wa taasisi mbalimbali wilayani Ludewa wakifuatilia kwa umakini maelezo wanayopewa na Mkuu wa Jeshi la polisi wilayani humo Deogratius Masawe wakati akitoa elimu kuhusu kufuata sheria na taratibu za mikopo.
Mkuu wa jeshi la polisi wilayani Ludewa (watatu kulia) akifuatiwa na Ofisa Uchunguzi wa TAKUKURU wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa mikopo wa taasisi mbalimbali wilayani humo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment