RUWASA WILAYA YA SINGIDA YAANZA KWA KASI UTEKELEZAJI MIRADI YA MAJI | Tarimo Blog


Mhandisi wa RUWASA Wilaya ya Singida Joel Kibusi (katikati mwenye miwani) na wataalamu wengine (upande wa kulia) akikabidhi mabomba yenye ukubwa tofauti kwa wananchi wa kijiji cha Mitula utakapotekelezwa mradi huo.
Mtaalamu wa Wakala  wa Maji  na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Singida  (RUWASA) , Mhandisi Joel Kibusi kwa niaba ya Meneja wa RUWASA Wilaya ya Singida, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mitula wakati wa hafla ya kupokea vifaa vitakavyotumika kwenye ujenzi wa mradi huo.
Mwonekano wa mabomba hayo.
Mtaalamu wa RUWASA Wilaya ya Singida Ernesta Kihwele, akielekeza jambo baada ya kupokea vifaa hivyo.


Wananchi na mmoja wa wataalamu wa RUWASA Abel Rusatila (wa pili kulia) wakiwa kwenye hafla hiyo.
Meneja wa Wakala  wa Maji  na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Singida  (RUWASA) , Mhandisi Athuman Mkalimoto akizungumza muda mfupi baada ya kupokea mabomba na vifaa  mbalimbali vitakavyotumika kutekeleza mradi wa maji wenye thamani ya zaidi ya milioni 316 kwenye Kijiji cha Mitula, Wilaya ya Singida jana.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa kupeana maelekezo ya namna ya utunzaji wa vifaa hivyo kabla ya kukabidhiwa na mwenendo mzima wa hatua kwa hatua ya utekelezaji wa mradi huo.
Mtaalamu wa RUWASA Wilaya ya Singida James Shija akifanya uhakiki wa vifaa hivyo.
 


Na Godwin Myovela, Singida


WAKALA wa Maji  na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Singida mkoani hapa (RUWASA) imeanza kwa kasi kutekeleza miradi mbalimbali ya usambazaji wa huduma za maji kwenye maeneo kadhaa yanayozunguka wilaya hiyo ikiwemo vijiji vya Mitula, Mwiganji, Migugu na Ughandi B ambavyo kwa muda mrefu vilikosa huduma hiyo muhimu.

Imeelezwa, kwa mujibu wa RUWASA Wilaya ya Singida zaidi ya wananchi elfu kumi wanaozunguka vijiji hivyo wanatarajia kuanza kupata maji safi na salama katika kipindi cha miezi mitatu mpaka mitano kuanzia sasa ikiwa ni utekelezaji wa miradi minne ya kibajeti 2021/2022 chini ya serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)

Akizungumza jana muda mfupi baada ya kushusha mabomba na vifaa vya mbalimbali vitakavyotumika kutekeleza mradi wa maji kwenye kijiji cha Mitula na maeneo mengine, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Singida, Mhandisi Athuman Mkalimoto, alipongeza kasi ya serikali na ushirikiano uliopo kwa namna ilivyojikita kwenye umakini kuhakikisha huduma za usambazaji maji vijijini zinaendelea kuimarika.

Meneja Mkalimoto alisema katika kutekeleza bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/22 RUWASA Wilaya ya Singida tayari imeanza kutekeleza mradi wa maji kijiji cha Mwighanji ambao mpaka kukamilika kwake unatarajia kutekelezwa kwa thamani ya shilingi milioni 500, huku mradi mwingine ambao tayari umeanza kutekelzwa kwa hatua za mwanzo ni wa kijiji cha Migugu kupitia fedha za ‘Uviko’ unaokwenda kunufaisha zaidi ya wananchi elfu 6 ambao una thamani ya shilingi milioni 565.

Alisema mradi mwingine wa kijiji cha Ughandi B mpaka sasa tayari umeshatekelezwa kwa zaidi ya asilimia 75 ya ujenzi wake, na alisisitiza kwamba kilichobakia ni ukamilishaji wa tenki la maji ili huduma zianze kupatikana.

“Kazi kubwa zote kwa maana ya chanjo, kuweka pampu, sola, vituo 11 vya kutolea maji sambamba na ujenzi wa tenki la lita elfu 90 juu ya mnara wa mita 12 lipo kwenye hatua ya mwisho ya ukamilishaji-tunatarajia kukabidhi mradi huu mapema Februari mwaka huu,” alisema Meneja Mkalimoto.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Ruwasa  Wilaya ya Singida, Joel Kibusi, pamoja na mambo mengine, alisema tayari wamepokea mabomba na vifaa vingine kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi mwingine wa maji safi na salama ndani ya kijiji cha Mitula ambao mpaka kukamilika kwake unatarajia kugharimu zaidi ya shilingi milioni 316.

Kibusi akizungumza na wananchi wa kijiji hicho alisema hatua ya kwanza kwa maana ya kupata chanjo kinachoweza kutosheleza mahitaji ya wakazi hao imekamilika na mkandarasi tayari amepatikana na ujenzi unatarajia kuanza ndani ya kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa.

“Mradi wa Mitula utaanza kutekelezwa ndani ya wiki mbili kuanzia sasa na utakamilika ndani ya miezi 2 mpaka mitatu. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na kujenga vituo 7 vya kuchotea maji ‘domestic points,’ tenki la maji lenye ujazo wa lita elfu 75 litakalojengwa juu ya mnara wa mita 6, tutaweka sola kisimani, ufungaji wa pampu mpya, uchimbaji na ulazaji mabomba na ujenzi wa nyumba ya mashine,” alisema Kibusi.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2