TAHA 'YAPIGA KAMBI' MAONESHO YA BIASHARA KUELEZEA WANAYOYAFANYA KUENDELEA KILIMO CHA HORTICULTURE | Tarimo Blog

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

SHIRIKA la Horticulture for Health and Wealth(TAHA)imewakikishia Watanzania kwamba inaendelea kufanya kazi ya kuimarisha tasnia ya kilimo cha horticulture kwa kuunganisha na kuratibu wahusika wa mnyonyoro wa wa thamani wa tasnia chini ya paa moja huku likisisitiza kilimo cha horticulture kinalipa.

Limekumbusha lengo kuu la TAHA ni kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo cha horticulture nchini Tanzania kwa ukuaji jumuishi hai na endelevu huku wakifafanua kuwa TAHA ni asasi kilele ya sekta binafsi ambayo inatetea ukuaji wa na ushindani wa sekta ya kilimo hicho nchini tangu kuanzisha kwake mwaka 2004.

Akizungumza leo katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea Viwanja vya Mwalimu Nyerere maarufu Sabasaba mkoani Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano kwa Wateja wa Shirika la TAHA Lovennes Adolf amesema wamekuwa jukwaa la kutoa sauti kwa wazalishaji, wafanyabiashara, wauzaji bidhaa nje na wasindikaji wa mazao ya horticulture kama maua, matunda , mbogamboga, mimea tiba , viungo na mazao yatokanayo na mizizi.

"Shirika linalinda masilahi ya sekta binafsi na kuhakikisha masuala ya sekta ya kilimo cha maua yanajumuishwa vizuri katika ajenda za kitaifa, kikanda na kimataifa,"amesema Adolf na kusisitiza inatekeleza shughuli zake za kibiashara ili kufikia malengo yake kwa kukuza na kuhuisha uzoefu katika sekta hiyo na kuongeza uimara wa kifedha wa shirika.

Akifafanua zaidi wakati akizungumza na vyombo vya habari kwenye maonesho hayo, Adolf ameeleza dira yao ni sekta mahiri ya uchumi, mafanikio na endelevu ya tasnia ya horticulture wakati dhima yao ni kusimamia ukuaji jumuishi, mabadiliko , ushindani na maendeleo ya sekta hiyo ya kilimo hicho nchini Tanzania.

Ameongeza katika kutekeleza dira na dhamira yao TAHA kwa kushirikiana na wadau wanaongozwa na madili sita ambayo ni uwazi, heshima kwa wote, uwajibikaji, kujali wateja, kuzingatia muda na wakati pamoja na uendelezaji na ujumuishaji.

Kuhusu uwepo wao kwenye maonesho hayo, Adolf amesema wanatambua umuhimu wa maonesho hayo na uwepo wao umesaidia kukutana na wananchi mbalimbali ambao wamekuwa wakifika kufahamu shughuli za TAHA na hivyo ni matumaini yao baada ya kumalizika kwa maonesho hayo watakuwa wamepata mabalozi ambao watakuwa mstari wa mbele kuelezea shughuli wanazozifanya kwani wao hawawezi kufikia wananchi wote.

Aidha amesema TAHA inaendesha kazi zake katika mikoa 25 nchini Tanzania Bara na Visiwani ambapo ametaja mikoa hiyo ni Arusha, Mwanza, Manyara, Kilimanjaro,Tanga,Dodoma,Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya , Pwani, Dar es Salaam , Lindi, Mtwara, Mara, Simiyu, Shinyanga, Singida , Songwe, Unguja Mjini/Magharibi, Kusini Unguja na Kaskazini Unguja,Kusini Pemba na Kaskazini Pemba.

"Tunatekeleza shughuli zetu kupitia mfumo wa kongani kama sehemu ya kufikia jamii ambazo zimelengwa kikamilifu hivi sasa.Tuna kongani 18 kwenye mikoa husika,"amesema Adolf na kuongeza TAHA imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali yanayolenga kumjengea mkulima uwezo wa kuzalisha mazao bora kwa kufuata kanuni na mbinu bora za kilimo.

Ameongeza katika kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na mazingira wezeshi ya biashara TAHA huainisha na kuchambua sera, kanuni na sheria zinazohusu kilimo na biashara ya mazao ya horticulture na kuishauri Serikali namna bora ya kuziboresha."Katika hili TAHA imefanikiwa kuishawishi Serikali kufanya mabadiliko mbalimbali ya kisera, kikanuni na kisheria kwa lengo la kuboresha mazingira wezeshi ya biashara nchini."

Wakati huo huo amesema miaka ya nyuma walikuwa wanashirikiana na kampuni nyingine ambao ni watoa huduma na wanachama wa TAHA ambao wamekuwa walikuwa wakitumia maonesho hayo kuonesha bidhaa zao kama mbegu, dawa na mbolea lakini mwaka huu wameona watoe nafasi kwa wajasiriamali wadogo ambao wanasindika bidhaa mbalimbali.

Ameongeza wajasiriamali ambao wamekuwa nao mwaka huu katika maonesho hayo ya biashara ya kimataifa wanatoka Tanzania Bara na Visiwani."Katika banda letu mwaka huu tunao wajasiriamali 10 ambao wamekuja na bidhaa tofauti zikiwemo viungo pamoja na matunda ambayo wameyachakata kwa ajili ya matumizi.

"Kwa hiyo ni fursa kwao na tunategemea kupitia maonesho haya watakuwa wamejitangaza na kuweza kupata biashara nyingi zaidi, na tunatarajia watatupa mrejesho huko wanakokwenda kuhusu biashara zao.

"Wengi wanaokuja banda la TAHA wanataka kujua tuko kwenye mikoa gani na huduma gani ambazo tunazitoa, wengi wanaokuja hapa sio kwamba ndio mara ya kwanza wanatuona bali wameshatusikia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.Mwitikio mkubwa sana kama nilivyosema watu wengi sio ndio wanatuona Sabasaba bali wanajua tunachokifanya na ujumbe wetu kwa mwaka huu, tunawambia horticulture inalipa, watu waingie kwenye kilimo hicho."


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2