Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amelitaka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC,) kuhakikisha inarudisha mkopo wa Shilingi bilioni 4.5 walizokopa katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kuzalisha viuatilifu.
Hayo aliyasema jana, alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya kuona shughuli zinazofanyika kiwandani hapo na kueleza kuwa uwekezaji huo ni zao la mkopo wa shilingi bilioni 4.5 tangu mwaka 2016, lakini hadi sasa mkopo huo umelipwa kwa kiasi kidogo na hadi sasa deni limefikia karibu shilingi bilioni nane.
Waziri Mhagama alisema kuwa fedha hizo zilizokopwa ni za wanachama ambapo kazi ya mfuko wa NSSF ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao na kueleza kuwa NDC wakiwa wadau walikopa NSSF fedha hizo ambazo ni za wanachama na zinahitajika kurudishwa.
Pia alisema kuwa, wameiagiza NSSF kuangalia ni kwa namna gani fedha hizo za wanachama zitarejeshwa kwa utaratibu uliowekwa ili fedha za wanachama ziweze kubaki katika utaratibu wa kulipa mafao muda unapofika.
Waziri Mhagama amesema wamekuwa wakiishauri NSSF kutowekeza au kuendesha viwanda wenyewe bali waangalie wanaweza kuingia ubia na nani, hivyo NDC tunawakumbusha kurejesha fedha hizo katika mfuko ili zikatekeleze majukumu waliyokusudia.
"Lakini NDC ni taasisi ya Serikali kwa hiyo Serikali inawajibu wa kuzungumza huko ndani, kuondoa vikwazo na kuhakikisha kwamba kiwanda kinaendelea kukuwa kama matarajio yalivyokubaliwa kwani kiwanda hiki ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, Pia wanatakiwa kuhakikisha kiwanda kinafanya kazi kutokana na umuhimu wake na faida tengamanishi kwenye Taifa letu." Amesema.
Kuhusiana na kero za wafanyakazi wa kiwanda hicho, Waziri Mhagama alisema, wameweka makubaliano kati ya Wizara yake Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuingilia kati ili kumaliza changamoto zinazowakabili kwa haraka sana.
Aidha alisema katika masuala mengine lazima Wizara zikutane na kutafuta suluhu za changamoto hizo na TAMISEMI wasaidie kwa kuhakikisha wanapambana na mbu wanaoeneza malaria kwa kutumia kiwanda hicho.
"Wizara ya Afya inatumia fedha nyingi sana kununua dawa za kutibu malaria, ni afadhali kutumia fedha kidogo kukinga ugonjwa wa malaria kuliko kuendelea kupoteza fedha kuagiza dawa za Malaria, Lakini tuna Wizara ya Mifugo, kiwanda hiki licha ya kutengeza viuatilifu kwenye eneo la mapambano dhidi ya malaria, tunaweza kutengeneza pia mbolea ambayo itatumika kwenye mazao yetu, lakini tunaweza kutengeneza chanjo ya wanyama mbalimbali.....Sasa Wizara ya mifugo inaweza kutengeneza chanjo hapa hapa, Wizara ya kilimo inaweza kutengeneza mbolea hapa, lakini Wizara ya Maliasili na Utalii inaweza kutengeneza chanjo kwa ajili ya wanyama ambao wako katika mbuga zetu hapa." Ameeleza.
Amewashauri Mawaziri kukutana haraka ili kujua hatma ya kiwanda hicho kinachotangaza Taifa katika ukanda wa Afrika kabla hakijafa wala kushindwa kutoa huduma iliyokusudiwa.
Kuhusiana na suala la masoko nje ya nchi Waziri Mhagama amesema tayari ametoa maagizo kwa NDC juu ya kufanya jambo la ziada la kutangaza kiwanda hicho nje ya nchi.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment