Na Mwandishi wetu, Babati
WATU 250 wanapata chanjo ya Uviko-19 Mkoani Manyara, kwa siku tofauti na awali ambapo idadi ilikuwa 66 kwa siku.
Mganga mkuu wa mkoa wa Manyara, Dkt Damas Kayera, ameyasema hayo mjini Babati kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo (RCC) wakati akielezea sekta ya afya.
Dkt Kayera amesema hivi sasa kuna mwamko tofauti na awali walikuwa wanachanjwa watu 66 kwa siku ila hivi sasa wanachanjwa watu250 kwa siku.
"Ongezeko hilo la watu kuchanjwa limekuja baada ya kuingia chanjo mpya ya Sinopharm, ambapo watu wengi wameichangamkia," alisema Dkt Kayera.
Amesema walipokea dozi mpya 35,766 na hadi hivi sasa wamechanja watu 6,112 kwenye Wilaya tano za mkoa wa Manyara.
Amesema mipango ya idara ya afya ni kuongeza kasi ya kuchanja hadi kufikia watu 1,000 kwa siku.
"Hali ikiendelea kuwa hivi itatuchukua muda wa miezi sita kufikia asilimia 60 ya malengo tuliyojiwekea," amesema Dk Kayera.
Amesema ushirikiano wa viongozi wa mkoa huo wa kisiasa, kidini na kimila ndiyo imekuwa chachu ya watu kuzidi kujitokeza kuchanja.
"Nawasihi wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya Uviko-19 kwenye mahospitali, vituo vya afya na zahanati.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere amewataka wananchi wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya Uviko-19.
Makongoro amesema ameshatoa maelekezo kwa viongozi wa ngazi ya Wilaya kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa taasisi ya afya ili wananchi wao washiriki chanjo.
Mganga mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt Damas Kayera akisoma taarifa ya afya kwenye kikao cha ushauri cha Mkoa huo (RCC) kilichofanyika Mjini Babati.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment